Waandamanaji wavinjari Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waandamanaji wavinjari Ukraine

Waandamanaji wa Ukraine wameingia wiki yao ya tatu ya kupinga uamuzi wa serikali ya nchi hiyo kukataa kufikia makubaliano ya kihistoria na Umoja wa Ulaya wakati Marekani ikionya juu ya uwezekano wa kuiwekea vikwazo.

Waandamanaji wakihami kambi yao katika uwanja wa uhuru mjini Kiev (11.12.2013)

Waandamanaji wakihami kambi yao katika uwanja wa uhuru mjini Kiev (11.12.2013)

Waandamanaji ambao wamekuwa wakiukalia uwanja wa uhuru katika mji mkuu wa Kiev kutokana na kukasirishwa na hatua ya serikali ya nchi hiyo kukataa makubaliano na Umoja wa Ulaya wamewalazimisha polisi kurudi nyuma kufuatia kushindwa kwa jaribio lao la kuvamia kambi ya wandamanaji hao mjini humo Jumatano alfajiri na hiyo kutowa pigo kwa mamlaka ya Rais Viktor Yanukovich.

Takriban watu 30 walijeruhiwa wakati polisi wa kutuliza ghasia na vikosi maalum vya wizara ya mambo ya ndani walipowavamia waandamanaji. Lakini masaa machache baadaye, Rais Yanukovich ameahidi serikali katu haitotumia nguvu nguvu dhidi ya maandamano ya amani na kuwataka wapinzani wakubali kukaa chini kwa mazungumzo.

Wito wa suluhu

Rais Victor Yanukovych wa Ukraine.

Rais Victor Yanukovych wa Ukraine.

Yanukovych amesema kwa matlaba ya kufikia muafaka anatowa wito kwa upinzani kutoyakataa mazungumzo hayo na kutofuata njia ya malumbano na kutowa amri. Amesema "Niko tayari kushiriki katika mazungumzo hayo mimi mwenyewe binafsi."

Shinikizo la kimataifa dhidi ya kiongozi huyo linazidi kuongezeka ambapo Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amekutana naye mara mbili hivi karibuni na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Victoria Nuland, akimweleza rais huyo jaribio la la polisi kuyavunja maandamano hayo kwa kutumia nguvu ni jambo lisilokubalika.

Vikwazo vyatafakariwa

Marekani imesema inafikiria hatua kadhaa za kuchukuliwa kutokana na hatua hiyo ya polisi ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Jen Psaki msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema wanafikiria hatua za kuchukuwa ikiwa ni pamoja na vikwazo ingawa bado hakuna uamuzi uliofikiwa. Waziri wa mambo ya ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ameionya serikali ya Ukraine dhidi ya kutumia nguvu za kijeshi kwa waandamanaji kwa njia yoyote ile na ameitaka iwe na subira. Katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa Ukraine Pavlo Lebedev, Hagel amesisitiza juu ya uwezekano wa kuwepo kwa madhara kwa kujihusisha kwa aina yoyote ile ya kijeshi katika kuvunja maandamano hayo dhidi ya serikali.

Waandamanaji waliovinjari katika uwanja wa uhuru mjini Kiev.(11.12..2013).

Waandamanaji waliovinjari katika uwanja wa uhuru mjini Kiev.(11.12..2013).

Waandamanaji zaidi 5,000 wamezidi kujiimarisha katika uwanja wa uhuru mjini Kiev walikokita kambi kwa kujaza theluji na michanga kwenye mifuko ya plastiki walioiweka kama uzio wa kujihami.

Upinzani umekuwa ukikataa kuwa na mazungumzo yoyote yale na Rais Yanukovich hadi hapo kiongozi huyo atakapoivunja serikali yake na kuwachukulia hatua ya kinidhamu polisi wa kutuliza fujo kwa kuvunja kwa nguvu maandamano ya madogo ya Novemba 30 na wameapa kufanya kila iwezalo kumpinduwa rais huyo. Waziri Mkuu wa zamani ambaye yuko gerezani Yulia Tymoshenko amelionya vuguvugu hilo la maandamano dhidi ya kufanya mazungumzo yoyote yale na Yanukovych.

Yanukovich anatarajiwa kwenda Urusi Disemba 17 kusaini makubaliano na Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo. Repoti pia zimedai kwamba viongozi hao wawili watakubaliana juu ya uwanachama wa Ukraine katika umoja wa forodha unaoongozwa na Urusi juu ya kwamba maafisa wa serikali ya Ukraine wamekanusha vikali jambo hilo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com