1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji 20 wameuwawa nchini Yemen

30 Mei 2011

Watu 20 wameuwawa baada ya vikosi vya usalama vya serikali ya Yemen kuwafyatulia risasi waandamanaji katika mji wa Taiz, kusini mwa nchi hiyo, na katika tukio lingine watu wanaohusishwa na mtandao wa Al-Qaeda wamewauwa

https://p.dw.com/p/11QdX
Polisi wakiwatawanya waandamanaji nchini YemenPicha: AP

Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, limemnukuu afisa mmoja akiwa katika hospitali mjini Taiz aliyesema kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na mamia ya watu waliojeruhiwa vibaya katika purukushani hizo.

Kwa upande wao, Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, linakadiria waliojeruhiwa kuwa ni takribani watu 150. Na kuongeza kuwa baadhi yao, kiasi ya watu 37, walichukuliwa na maafisa wa usalama kutoka hospitali.

Protests in Yemen am 18.02.2011
Mapigano kati ya wanaounga mkono serikali na wanaoipingaPicha: Picture-Alliance/dpa

Kwa mujibu wa mashahidi, usiku wa kuamkia leo polisi waliwafyatua risasi,mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji waliokusanyika nje ya jengo la manispaa mjini Taiz. Watu hao walikuwa wakishinikiza kuachiwa huru kwa wenzao waliokamatwa.

Waandamanaji wanasema polisi waliwatawanya wakati walipokusanyika katika uwanja wa ukombozi kwa kuwashambulia pamoja na kuwatia kizuizini waandishi habari kadhaa.

Taarifa hiyo ya Muungamo wa Upinzani imesema uhalifu huo hautasahaulika,wanaufuatilia na kuweka kumbukumbu na kwamba wote waliohusika, na hasa waliotoa silaha na fedha, hawatakwepa mkono wa sheria.

Katika tukio lingine, watu wanaohisika kuwa ni wafuasi wa mtandao wa kigaidi wa Al- Qaeda wamewauwa wanajeshi wanne wa Yemen na kuwajeruhi wengine kiasi saba baada ya kulivamia kundi hilo la wanajeshi huko kusini mwa mji wa Zinjibar.

Taarifa ya serikali ya Yemen inaesema kundi la wanajeshi hao lilishindwa kuhimilii kishindo cha kundi hilo la Al-Qaeda katika eneo la umbali wa kilometa moja kutoka mji wa Zinjibar.

Taarifa hiyo imesema miongoni mwa waliouwawa yumo Kanali wa Jeshi la Yemen.

Aidha katika muendelezo wa tukio kama hilo,watu wengine wanaohisishwa kuwa ni wafuasi Al-Qaeda wameuwawa katika mapambano kati yao na wanajeshi wa serikali katika maeneo ya mji wa Zinjibar.

Kundi linalohisiwa kuwa ni la Al-Qaeda linaushikilia mji wa Zinjibar, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Abyan, na ambao umekuwa na mapigano kwa zaidi ya siku tatu sasa, na ambayo yamesababisha vifo vya watu 21.

Kumekuwepo maandamano katika maeneo tofauti mjini Yemen ambayo shabaha yake ni kumshinikiza rais Ali Abdullah Saleh wa nchi hiyo ajiuzulu.

Maandamano hayo ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa sasa yamekuwa yakikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/ RTR

Mhariri: Miraji Othman