1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafghanistan hawajaridhika na shughuli za vikosi vya kimataifa-ISAF .

Oumilkher Hamidou7 Desemba 2010

Vikosi vya kimataifa vya kulinda amani nchini Afghanistan-ISAF vinaonyesha kupoteza imani ya wananchi wa Afghanistan,miaka tisaa tangu walipoingia nchini humo.

https://p.dw.com/p/QRLy
Jenerali David Petraeus,mkuu wa vikosi vya ISAF nchini AfghanistanPicha: AP

Jinsi wananchi wa Afghanistan wanavyowaangalia wanajeshi wa kimataifa wa kulinda amani nchini mwao- ISAF,dhamiri za kuhamishiwa nchini Urusi takataka za kinuklea za Ujerumani na muda wa mapumziko anaostahiki kupata mama mjamzito anapokaribia kujifungua.Hayo ni miongoni tuu mwa yale yaliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanze basi na Afghanistan ambako imani ya wananchi kuelekea vikosi vya kulinda amani vya kimataifa-ISAF inasemekana imepungua sana.Gazeti la "DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN" linaandika:"Ni sura mbaya kabisa wanayopewa wanajeshi wa kimataifa wanaoongozwa na jumuia ya kujihami ya NATO,licha ya kusalia miaka tisaa nchini humo.Vikosi hivyo vya kigeni vimeshindwa kujipatia imani ya wananchi.Imani hiyo lakini ndio msingi wa opereshini yote hiyo,kwasababu usalama na ujenzi mpya unawezekana tuu kwa ushirikiano pamoja na wananchi wa Afghanistan.Kinachotisha zaidi ni ile hali kwamba waachache tuu kati yao ndio wanaothamini shughuli za mashirika ya kimataifa ya misaada-kwasababu misaada mingi inamezwa na walarushwa serikalini.Wananchi wako mbali na kujivunia mfumo wa demokrasia, neema au usalama nchini Afghanistan."

Castortransport unterwegs nach Gorleben
Treni maalum inayosafirisha makontena yaliyosheheni takataka za kinuklea ikielekea katika kituo cha GorlebenPicha: dapd

Mada yetu ya pili magazetini inahusiana na mvutano wa wapi zihamishiwe takataka za kinuklea za Ujerumani.Gazeti la "Münchner Merkur" linaandika:"Kutokana na yote watu wanayoyasikia na kuyaona kuhusu jinsi takataka za kinuklea zinavyotupwa nchini Urusi,kila mwenye busara hatokosea akisema laa,takataka zilizosheheni miale ya kinuklea kutoka magharibi zisipelekwe mashariki.Waziri wa mazingira wa serikali kuu ya Ujerumani,Norbert Röttgen hajakosea kwa hivyo alipoamuru makontena yaliyosheheni takataka za kinuklea yasisafirishwe hadi Majak nchini Urusi.Msafara kama huo mwisho wake hakuna anaeweza kuukadiria."

Gazeti la "Ostsee-Zeitung" linahisi bora takataka hizo za kinuklea zingesalia humu humu nchini japo kwa muda.Gazeti linaendelea kuandika:"Takataka za kinuklea za Ujerumani Mashariki ya zamani hazitomwagwa katika vyoo vya Urusi.Zitasalia katika ardhi ya Ujerumani,angalao kwa muda.Kwasababu waziri wa mazingira wa serikali kuu hajaifunga milango yote.Anasema ikiwa hali itabadilika nchini Urusi,maombi ya kusafirishwa kwa meli takataka za kinuklea yanaweza pia kutolewa."

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu muda wa maoumziko wa mama mjamzito,kabla hajajifungua.Gazeti la"Oldenburgische Volkszeitung linaandika:"Tatizo linakutikana kutokana na ile hali kwamba halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya haijafikiria vizuri-wanataka mama mjamzito apumzike kwa muda wa wiki 18 na kupokea mshahara timamu-Bunge la Ulaya linakwenda mbali zaidi linataka mama mjamzito aruhusiwe kubakia wiki 20 nyumbani.Kwa hivyo ni jambo linaloingia akilini ikiwa waziri wa familia wa serikali kuu Kristina Schröder anapinga fikra hiyo na kuzungumzia juu ya muda wa mapumziko anaopata mama mjamizito nchini Ujerumani-yaani wiki 14.Lakini pingamizi pekee hazitoshi -waziri wa familia wa serikali kuu ya Ujerumani angebidi pia kuwafafanulia wenzake katika Umoja wa Ulaya msingi wa utaratibu unaotumika nchini Ujerumani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mpitiaji:Abdul-Rahman,Mohammed