1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyumba vyapanda bei London

Thelma Mwadzaya28 Aprili 2011

Mjini London, wenye nyumba wanajiandaa kuitumia fursa hii ya harusi ya Kifalme kuwapangishia wateja kwa bei za juu. Harusi ya Kifalme ya Mwanamfalme William na Kate Middleton imepangwa kufanyika tarehe 29 mwezi wa Aprili

https://p.dw.com/p/115B7
Mtaa wa mji wa LondonPicha: picture-alliance/dpa


 Shughuli hiyo imewalazimu wageni na watalii wanaotaka kulishuhudia tukio hilo la kihistoria kutafuta mahala pa kukaa kwa muda. Taarifa zinaeleza kuwa hoteli kote mjini humo zimejaa pomoni na kwa sasa wageni wanatafuta nafasi katika majumba ya watu binafsi.

Kulingana na maelezo, watalii wanaotokea sehemu tofauti kote ulimwenguni wako tayari kulipa ada yoyote ile watakayotozwa na wenye nyumba kokote kule. Inaaminika kuwa wenye nyumba hao huenda wakajikusanyia kiasi ya euro milioni 114 kama ada ya kuwapangishia wateja katika msimu huu wa shamrashamra. 

UK London Großbritannien William Kate Hochzeit Camper
Wageni na watalii wanaomiminika London kulishuhudia tukio la KihistoriaPicha: AP

Mandhari ya kuvutia

Bei ya vyumba vya nyumba zilizoko maeneo ya ufuoni mwa Mto Thames zinaripotiwa kuwa juu kwani mandhari hayo ya Daraja ya Tower na bustani yanavutia. Kwa mujibu wa wataalam wanaohusika na biashara ya kupangisha na kuuza nyumba, bei ya vyumba vya hoteli ambazo zimeongezeka na uhaba wa nafasi kwa jumla vimezifanya ada za nyumba kuongezekea kwa asilimia 40.

Mtaalam mmoja wa Kampuni ya kupangisha nyumba ya Find a property anasema kuwa harusi hii ya Kifalme inafanyika katika kipindi ambacho wadau wa sekta hiyo hawakuwa wamejiandaa kujikusanyia ada kwa wingi. Takwimu zinaeleza kuwa kwa sasa hivi kila mgeni au mtalii anajitahidi kutafuta pa kueka kichwa tu…hata kochini.

Queen`s Gallery Buckingham Palace London
Kasri la BuckinghamPicha: picture-alliance/dpa

Euro 34 hadi alfu 4

Bei za vyumba hivyo zinanzia kati ya euro 34 kwenye nyumba za binafsi hadi euro alfu 4 kwa wiki moja ili kuipangisha nyumba nzima kwenye eneo lililo katikati ya mji wa London.

Kwa kawaida, hakuna sheria maalum inayomzuwia mwenye nyumba kuwatoza wapangaji wake kodi ya juu. Hii ina maana kuwa wana uhuru wa kufanya wanachokiona sahihi ukizingatia kuwa mahitaji ya nyumba na vyumba yameongezeka katika kipindi hiki.

Tathmini zinaeleza kuwa watalii na wageni wengi watakaoshuhudia harusi hiyo ya Kifalme wanatokea Ujerumani, Japan na Marekani.

Harusi hii ya Kifalme pia inawaandaa wenye nyumba wanapoisubiri michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2012.