Vyombo vya habari vina dhima kubwa kwenye uchaguzi | Tanzania Yaamua 2015 | DW | 25.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Tanzania Yaamua 2015

Vyombo vya habari vina dhima kubwa kwenye uchaguzi

Wadau wa tasnia ya habari nchini Tanzania wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili namna wanavyoweza kutoa mchango wenye tija katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Mkutano huo ambao pia ulijumuisha viongozi wa kidini pamoja na washiriki kutoka katika baadhi ya mataifa jirani umefungua ukurasa wa majadiliano yanayotaka vyombo vya habari kutoa mchango chanya kufanikisha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 25.

Akizungumza katika mkutano huo, mwanadiplomasia mmoja mwandamizi kutoka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya alisema kuwa "Ulaya inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kujenga taifa lenye ustawi wa kidemokrasia na maendeleo kwa raia wote," akiongeza kwamba Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na mataifa ya Afrika ili kudumisha demokrasia na amani.

Kwa upande wake, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilizungumzia haja ya kuwa na vyombo vya habari vyenye kuzingatia weledi hasa katika wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu. Afisa mwandamizi wa jumuiya hiyo alisema kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari "kunatoa mustakabali mwema kwa ujenzi wa taifa lenye kuwajibika, kwani vyombo hivyo vina karata muhimu ya kufanikisha uchaguzi mkuu na hivyo akataka uhuru wa vyombo vya habari uzingatiwe.

Baadhi ya washiriki waliochagia mada kwenye kongamano hilo la siku mbili walihimiza juu ya kile walichokiita mashirikiano ya dhati baina vyombo vya habari na taasisi za maamuzi ikiwamo serikali yenyewe.

Hoja kama hiyo ilijitokeza pia kwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari, Reginald Mengi, ambaye yeye alikwenda mbali zaidi akisema kuwa "amani ya taifa iliyopo sasa ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa katika siku za nyuma hivyo kila mmoja anapaswa kutetea na kuilinda."

Washiriki wa kongamano hilo watatoa maazimio yao mwishoni mwa mkutano wao hapo siku ya Alhamisi.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com