Vurugu zimeendelea Sudan Kusini licha ya mkataba wa amani | Matukio ya Afrika | DW | 19.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Vurugu zimeendelea Sudan Kusini licha ya mkataba wa amani

Ripoti mpya ya tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema kiwango cha vurugu ni kibaya zaidi Sudan Kusini kuliko ilivyokuwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na zinachochewa na maafisa wa ngazi ya juu

Ripoti hiyo mpya kuhusu haki za binadamu nchini Sudan Kusini iliyotolewa leo, inaonya kwamba raia wapo katika hatari kubwa ya mauaji na madhila mengine ikiwemo ubakaji, kukosa makaazi na kutekwa. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2018 nchini humo viliwaua watu takribani 400,000 na mamilioni wengine bado hawasahau taabu walizopitia.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Yasmin Sooka amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva kwamba "vurugu zimeendelea kwa sababu watu wanajua hawawezi kuwajibishwa." Mwenyekiti huyo anaamini kwamba uratibu wa machafuko hayo unatoka ngazi ya juu.

Msemaji wa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema anahitaji kusoma ripoti hiyo kabla ya kutoa kauli yoyote, ingawa kaimu msemaji wa jeshi Santo Dominic Chol amesema kwamba hii sio mara ya kwanza tume kutoa ripoti ya namna hiyo.

"Hatupingi ripoti yenu, lakini tungependa mtupatie ripoti hiyo ili kama kuna maeneo ambayo taasisi zetu zimefanya makosa tuweze kurekebisha", alisema kaimu huyo msemaji wa jeshi.

Südsudan Verhandlungen zwischen Regierung und Opposition

Viongozi wa Sudan Kusini Salva Kiir na makamu wake Riek Machar

Ripoti ya leo inaelezea mashambulizi dhidi ya raia kuwa yanafanywa kwa misingi ya kikabila na wakati mwingi yanaungwa mkono na vikosi vya taifa na upinzani. Kulingana na ripoti hiyo, mamia ya watu waliuawa kati ya Februari na Novemba mwaka jana pekee.

Ripoti hiyo inatolewa mwaka mmoja baada ya serikali ya Umoja wa Kitaifa kuundwa Sudan Kusini baina ya kiongozi wa zamani wa waasi Riek Machar ambaye sasa ni makamu wa rais wa Salva Kiir. Lakini kwa zaidi ya miaka miwili tangu makubaliano ya amani yasainiwe ya kumaliza vita, utekelezaji zaidi umekuwa ukisuasua.

Mapigano mapya yalianza muda mfupi baada ya mkataba wa amani kusainiwa na yameendelea kuyakumba maeneo ya Equatorial ya Kati, Jonglei, Warrap na Pibor. Baadhi ya maeneo yaliyoathirika pia yameharibiwa vibaya na mafuriko, huku maelfu ya watu wakikosa makaazi na kiwango cha njaa katika baadhi ya maeneo kinaelekea kuwa baa la njaa.

Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema wapiganaji wanashindana kwa ajili ya kudhibiti madaraka na rasilimali, wakati baadhi ya maeneo nchini humo yakikosa usalama. Sooka anaendelea kusema kwamba "uhamasishaji wa maelfu ya wapiganaji wenye silaha za kisasa unaratibiwa vizuri na umekuwa wa kijeshi na sio kwa bahati mbaya.''

Matumizi mapya ya silaha na kiwango cha mapigano vinaashiria "ama ushiriki wa vikosi vya usalama vya taifa au wapiganaji kutoka nje", alisema afisa mwingine wa tume ya haki za binadamu.