1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu Pakistan

14 Mei 2009

Vita vya kupambana na watalibani na kuimarisha Afghanistan.

https://p.dw.com/p/HqQ0

Pakistan ina uwezo wa kuwashinda wataliban kwa nguvu za kijeshi,lakini yamkini ikashindwa vita vya kuuridhisha umma wake endapo haitaweza kuwasaidia maalfu ya wananchi wake waliokimbia maskani yao kutokana na mapigano-hii ni kwa muujibu wa waziri mkuu Yusuf Raza Gilani alivyosema leo.

Jeshi la Pakistan lilianzisha hujuma kali katika Bonde la Swat,kaskazini-magharibi mwa mji mkuu Islamabad wiki iliopita .Hii ilifuatia tuhuma za Marekani kuwa serikali ya Pakistan-dola lenye kumiliki silaha za nuklia linaiachia mamlaka wafuasi wenye itikadi kali.Si chini ya watu 830.000 wamehama nyumba zao na kujiunga na kundi jengine la watu nusu-milioni waliokimbia mapigano huko kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Kamishna wa UM anaehusika na wakimbizi Antonio Guterres, akizuru kambi moja ya wapakistan waliokimbia maskani yao,alisema kuwa Pakistan inahitaji msaada mkubwa wa kimataifa ili kuepusha msiba.Nae waziri mkuu Gillani amsema kwamba ,serikali ya Pakistan inapanga kuitisha mkutano wa wafadhili ,lakini pia anawatarajia wananchi wa Pakistan pia kusaidia.

Sehemu kubwa ya vyama vya kisiasa nchini Pakistan inaungamkono hujuma za kupambana na watalibani licha ya kuwepo shaka shaka nyingi juu ya kuwa na usuhuba mkubwa na Marekani.Mashambulio dhidi ya watalibani yalianzishwa pale rais Asif Ali Zardari alipokuwa ziarani mjini Washington kumhakikishia mshirika wake Marekani kwamba serikali yake haikaribii kuanguka na imejitolea kweli kupambana na wafuasi wenye itikadi kali.

Hujuma za Pakistan dhidi ya wapiganaji wenye siasa na itikadi kali huko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo,ni muhimu sana katika juhudi za Marekani za kuishinda Al Qaeda na kuiimarisha nchi jirani ya Afghanistan.Kikosi cha askari 15.000 kinapambana na wapiganaji 5,000 wenye siasa kali mkoani Swat.

Uingereza jana iliiahidi Pakistan kushirikiana nayo barabara katika kupambana na ugaidi na kuipa msaada wa maendeleo wa kiuchumi katika vita dhidi ya watalibani.Wakati wa mazunguzmzo mjini London , Rais Asif Ali Zardari na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown, walitunga mipango ya mkakati ulioongoza kufanyika ziara ya Brown nchini Pakistan.Maafisa wa uingereza wanasema wana masilahi ya kibinafsi katika kuisaidia pakistan kupambana na wenye siasa kali kwavile kiasi cha thuluthi-mbili ya njama za ugaidi nchini mwake zina mafungamano na Pakistan.

Mwandishi :Ali,Ramadhan/ RTRE

Mhariri:M.Abdul-Rahman