1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu dhidi ya wageni zatisha Afrika Kusini

17 Aprili 2015

Umoja wa Mataifa umezungumzia wasiwasi wake kuhusu hali mpya ya mashambulizi dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini ukisema ghasia zimesababisha raia wa kigeni 5000 kuachwa bila makaazi

https://p.dw.com/p/1FADX
Wahamiaji wakiafrika waliobeba silaha kujilinda kabla ya kutawanywa na polisi,Johannesburg
Wahamiaji wakiafrika waliobeba silaha kujilinda kabla ya kutawanywa na polisi,JohannesburgPicha: Reuters/S. Sibeko

Vurugu na mauaji dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini zimesambaa kutoka mji wa bandari wa mashariki wa Durban hadi mji mkuu wa kiuchumi wa taifa hilo Johannesberg katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Shirika linaloshughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetoa taarifa likisema zaidi ya watu 5000 raia wakigeni wakiwemo wakimbizi wameachwa bila mahala pa kuishi nchini humo hali ambayo inatia wasiwasi mkubwa .

Mkimbizi akifua katika Kambi ya wakimbizi mjini Durban
Mkimbizi akifua katika Kambi ya wakimbizi mjini DurbanPicha: picture alliance/dpa/Str

Shirika hilo limesisitiza kwenye taarifa yake kwamba walioathirika katika vurugu hizo za mashambulizi dhidi ya wageni ni wakimbizi na wanaoomba hifadhi ambao wamelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita na kukhofia kukamatwa na kushtakiwa na kwahivyo wapo Afrika Kusini kwasbabi wanahitaji kulindwa.

Katika muda wa wiki mbili zilizopita maduka pamoja na majumba yanayomilikiwa na wasomali,Waethiopia,wamalawi na wahamiaji wengine mjini Durban na vitongoji vyake zimelengwa katika mashambulio hayo ya ubaguzi na chuki dhidi ya wageni hali iliyozilazimu familia nyingi kukimbilia makambi yanayolindwa na walinzi wenye silaha .

Maduka ya wageni katika mji wa Jeppes katikati ya mji mkuu Johannesberg pia yameshambuliwa.Wisdom Dike ni mhamiaji anayefanya kazi kutoka Nigeria anaitaka serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua zaidi kuwalinda watu kama yeye ambao biashara zao zimevamiwa na kuharibiwa.Dike anasema tunanukuu,

''Wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi tuliisaidia Afrika Kusini na sasa tunaitaka serikali kutuelewa na kufahamu kwamba sisi ni kitu kimoja.''

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP polisi leo kwa mara nyingine wamemiminika kwa wingi mitaani baadhi wakifyetua risasi za mpira kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliokusanyika nje ya bweni wanamoishi wafanyakazi wakigeni la Jeppe mjini Johannesberg.

Baadhi ya wafanyakazi hao wamedai kwamba polisi walifyetua risasi usiku bila sababu huku wakiwatuhumu wageni kwa kuwapora watu katika eneo hilo.Ikumbukwe kwamba wenyeji na wahamiaji nchini humo mara kwa mara hushindania ajira hali ambayo mara zote inawafanya wageni kulengwa katika vurugu za aina hii pamoja na uchokozi mwingine.Mwaka 2008 watu 62 waliuwawa katika vurugu na ghasia zinazotokana na chuki dhidi ya wageni katika mitaa ya mji wa Johannesberg.

Ghasia hizi mpya zinazoshuhudiwa zilizuka baada ya mfalme wa Zulu Goodwill Zwelithini kutoka matamshi yaliyotangazwa na vyombo vya habari vya ndani yaliyodaia kwamba wageni wanapaswa kuondoka Afrika Kusini.Hata hivyo tangu wakati huo amenukuliwa kusema kwamba kauli yake imetafsiriwa vibaya.

Maandamano ya amani kupinga vurugu mjini Durban,Alhamisi
Maandamano ya amani kupinga vurugu mjini Durban,AlhamisiPicha: Getty Images/Afp

Ghasia hizo zimeendelea kupingwa duniani.Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS imelaani mauaji na vurugu hizo ikisema ni kitendo kilichopitwa na wakati,cha kihalifu na mauaji ya chuki dhidi ya wageni wasiokuwa na hatia nchini humo.Jumuiya hiyo Imeitaka serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua za haraka kukomesha kuongezeka kwa wimbi hilo la mashambulizi nchi nzima.

Rais wa Ghana John Dramani Mahama akitoa taarifa kwa niaba ya ECOWAS kama mwenyekiti wake amesema Afrika Kusini inabidi itambue wanaouwawa kwa kuonekana ni watu kutoka nje ni watu ambao nchi zao zilijitolea kuwasaidia waafrika Kusini kupambana,kuzuia na kuushinda ubaguzi wa rangi.Mapema wiki hii Malawi ilitangaza itawaondoa raia wake wanaishi Afrika Kusini.Alhamisi mamia ya watu waliandamana hadi ofisi za ubalozi wa Afrika Kusini mjini Harare Zimbabwe kupinga mashambulizi hayo. Afrika Kusini kupitia waziri wake wa mambo ya nje Maite Nkoana-Mashabane aliyekuwa na mkutano na wanadiplomasia wa kiafrika mjini Pretoria, imeomba uungaji mkono wa kidiplomasia wa nchi za Kiafrika kukabiliana na hali hii.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFP/DPA

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman