1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuguvugu la Azadi lapania kuipundua serikali ya Pakistan

Oumilkheir Hamidou
1 Novemba 2019

Malaki ya wanaharakati kutoka vyama vya upinzani vya Pakistan wamepiga kambi katika mji mkuu wa nchi hiyo Islamabad kwa lengo la kumlazimisha waziri mkuu Imran Khan ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/3SKZE
Pakistan Islamabad | Anti-Regierungsproteste
Picha: DW/I. Jabeen

Shule zimefungwa kwa siku ya pili mfululiizo na msongamano wa magari ukivuruga shughuli za mji huo huku wanajeshi 17,000 wakisambazwa kulinda amani.

Licha ya vizuwizi katika baadhi ya njia kuu waandamanaji waliojazana ndani ya mamia ya magari na mabasi wakiongozwa na Maulana Fazul Rehman mkuu wa chama cha Kiislam cha Jamiat-Ulema-e-Islam wamejipenyeza mjini Islamabad alfajiri wakisubiri amri kutoka kwa viongozi wao kabla ya sala ya Ijumaa.

Rehman  ameongozana na vuguvugu hilo wanaloliita " Vuguvugu la Azadi" Au Vuguvugu la Uhuru kutoka mji wa kusini wa Karachi tangu jumapili iliyopita na kuzunguka masafa ya kilomita 2000 hadi kuwasili mji mkuu Islamabad saa sita za usiku, alkhamisi.

Makundi mengine ya upinzani likiwemo lile la rais wa zamani Asif Ali Zardari na waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif nayo pia yamejiunga na maandamano hayo na kuzidi kumtia kishindo waziri mkuu Imran Khan.

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan
Waziri mkuu wa Pakistan Imran KhanPicha: picture-alliance/AA/Iranian Presidency

Waandamanaji wanasema uchaguzi wa mwaka jana ulikuwa wa hadaa

Rehman, shekhe wa miaka 66  anaetokea katika Chuo cha mafunzo ya kiidini- ya madhehebu ya Sunni  cha Deobandi chenye ushawishi mkubwa anamtaka Imran Khan ajiuzulu au akabiliane na wimbi la maandamano la malaki ya wafuasi wake. "Tunakwenda Islamabad kuipindua serikali haramu" alisema Rehman alipowasili karibu na mji mkuu Islamabad.

Waandalizi wa maandamano hayo hawakuwaruhusu wanawake kushiriki na kuzusha lawama katika mitandao ya kijamii.

Vyama vya upinzani vinasema uchaguzi wa mwaka 2018 uliomleta madarakani Khan ulifanyika kutokana na ushawishi wa jeshi na matokeo yake yalikuwa ya hadaa yakilenga kuileta madarakani serikali wanajeshi waliokuwa wanaitaka.

Wanajeshi waliitawala Pakistan kwa takriban nusu ya muda wote tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947.

"Tumetoka ili kushindana na serikali inayotumwa na wanajeshi" msemaji wa Rehman, Ghafoor Haider amesema.

Waziri mkuu Imran Khan anakataa kujiuzulu licha ya malalamiko kuhusu ughali wa maisha.