1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen ateuliwa katika wadhifa wa juu zaidi Ulaya

Daniel Gakuba
3 Julai 2019

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii (03.07.2019) wamezungumzia kuteuliwa kwa waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Ursula von der Leyen katika wadhifa wa juu kabisa kwenye Umoja wa Ulaya; urais wa Halmashauri ya umoja huo.

https://p.dw.com/p/3LVEo
Ursula von der Leyen CDU Verteidigungsministerin Deutschland
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Gazeti la Berliner Morgenpost limeandika kuwa uteuzi huo ni ahueni kwa Kansela Angela Merkel, ambaye alionekana kupoteza matumaini ya kumuona Mjerumani akiiongoza halmashauri hiyo. Gazeti hilo linashangilia namna Ujerumani inavyoonesha njia kwa kuwapa fursa wanawake. Baada ya Merkel kuwa kansela wa kwanza, sasa inaelekea von der Leyen atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Halmashauri ya Ulaya.

Baadhi ya wahariri, hata hivyo, wanaelezea kutoridhishwa na uteuzi huo wa von der Leyen. Mhariri wa gazeti la Straubinger Tagblatt anasema uteuzi wake haukufanyika katika mazingira mazuri. Anasema kuzuia mgombea wa kambi iliyopata kura nyingi katika uchaguzi ni sera mbaya, sawa na ujinga wa makundi yanayopinga Umoja wa Ulaya wa kung'ang'ania milele katika msimamo wao.

Tajiriba ya kimataifa

Maoni ya gazeti hilo ni kwamba itakuwa jukumu la Bunge la Ulaya, ambalo ndilo litamuidhinisha rasmi von der Leyen, kurekebisha pale viongozi wa Umoja wa Ulaya walipokosea. Gazeti hilo linamalizia kwa kulalamikia tabia iliyojitokeza katika mkutano wa kilele wa umoja huo, ya viongozi kuwekeana vizuizi kwa misingi ya kijinga na ya uzalendo, ilikisema tabia hiyo inapaswa kukomeshwa.

Sifa kuu inauhalalisha uteuzi wa Ursula von der Leyen, ni uzoefu wake kwenye ngazi ya kimataifa, ndivyo linavyoanza uhariri wake gazeti la Schwaebische-Zeitung, likizingatia kwamba mama huyo kabla ya kuwa waziri wa ulinzi wa Ujerumani, alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Kujihami, NATO.

Linasema bila kujali matokeo ya kura katika Bunge la Ulaya, kumuidhinisha au kumkataa von der Leyen katika wadhifa wa rais wa Halmashauri ya Ulaya, Kansela Merkel anapaswa kuitumia fursa hii kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, ambalo gazeti hilo linasema linao wajumbe kadhaa waliodhihirisha udhaifu kupindukia.

Kuachiwa kwa nahodha Rackete-Haki imeshinda

Mada nyingine iliyoangaziwa na magazeti ya Ujerumani katika uhariri wake ni kuachiwa huru kwa Carola Rackete, nahodha wa meli ya uokozi wa baharini iitwayo Sea Watch 3. Bi Rackete alikuwa amekamatwa nchini Italia baada ya kuipeleka meli yake iliyobeba wahamiaji kwenye bandari ya Lampedusa nchini Italia bila kibali cha kutia nanga.

Gazeti la Nordwest-Zeitung linasema uungwaji mkono alioupata Bi Rackete kutoka kwa raia wengi wa Ulaya, kupitia michango ya fedha na mikesha ya mshikamano, ni ujumbe mzito kwa serikali ya sera kali za mrengo wa kulia inayoongoza Italia.

Vuguvugu la mshikamano na nahodha huyo kutoka Ujerumani, linasema gazeti hilo, ni mapambano ya amani dhidi ya siasa zinazochipuka katika baadhi ya nchi za Ulaya zenye kuendekeza chuki dhidi ya wakimbizi na kujifungia ndani ya mipaka ya mataifa.

Mtazamo kama huo unapigiwa debe pia na gazeti la Passauer Neue Presse, ambalo linasema kitendo cha kibinadamu cha kuwanusuru wakimbizi kuzama baharini alichokifanya Nahodha Carola Rackete ndio hatua pekee ya kibinadamu mbayo inaweza kuchukuliwa.

Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo nasema ni jukumu la viongozi wa Ulaya kuweka sera muafaka ya kudhibiti mmiminiko wa wakimbizi wanaopitia katika njia hatari ya Bahari ya Meditarania, vinginevyo, sakata kama hili la kukamatwa na kuachiwa kwa Carola Rackete, halitachelewa kujitokeza tena.

DPA inlandspresse