1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen afanya ziara Kyiv kwa mazungumzo na Zelensky

15 Septemba 2022

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya amewasili mjini Kyiv leo Alhamisi kwa ziara yake ya kwanza nchini Ukraine tangu nchi hiyo iliyokumbwa na vita kupewa hadhi ya kuwania uwanachama wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/4Gw3n
Ukraine Ursula von der Leyen und Volodymyr Zelenskyy
Picha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Ziara ya rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen mjini Kyiv inatokea sambamba na mkutano kati ya viongozi wa Urusi na China unaofanyika nchini Uzbekistan, ambayo ni mwanachama wa zamani wa uliokuwa muungano wa Kisovieti.

Urusi na China zimesema mkutano huo wa kilele wa kikanda unatoa fursa mbadala ya kuupunguza ushawishi wa mataifa ya Magharibi ulimwenguni.

Soma pia:Ukraine yaendelea kurejesha maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi 

Mkutano huo kati ya marais Xi Jinping na Vladimir Putin unatokea wakati wanajeshi wa Ukraine wanaripotiwa kupata mafanikio katika uwanja wa mapambano dhidi ya vikosi vya Urusi hasa upande wa mashariki wa nchi hiyo.

Von der Leyen amesema leo kuwa, ziara yake ilikuwa ya tatu kuifanya nchini Ukraine tangu Urusi ilipoivamia mnamo mwezi Februari, japo amesisitiza kuwa ziara ya leo ni tofauti na za awali.

Ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii, "Mengi yamebadilika. Ukraine sasa imepata hadhi ya kuwa mgombea wa Umoja wa Ulaya." 

Ameongeza kuwa atajadiliana na Rais Volodymyr Zelenksy na Waziri Mkuu Denys Shmygal juu ya jinsi ya kuendelea kuimarisha uchumi wa Ulaya na kuwaleta Waukraine karibu wakati nchi hiyo ipo kwenye mchakato wa kutawazwa rasmi kuwa nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Ukraine ilipata hadhi ya kuwa mgombea wa kujiunga na Umoja wa Ulaya mnamo mwezi Juni wakati sawa na Moldova ambayo pia ni nchi mwanachama wa uliokuwa muungano wa Kisovieti, na ambayo inapakana na Ukraine.

Kura hiyo ya kihistoria iliikasirisha sana Urusi, ambayo inajaribu kwa udi na uvumba kupanua ushawishi wake wa kisiasa na kijeshi katika nchi hizo mbili-Ukraine na Moldova, tangu kusambaratika kwa muungano wa Kisovieti yapata miongo mitatu iliyopita.

Ukraine ina matumaini kutokana na mafanikio ya jeshi lake katika eneo la mashariki la Kharkiv 

Ukrainische Polizisten patrouillieren in der Gegend in der Stadt Izium
Wanajeshi wa Ukraine wakipiga doria katika mji wa Izium uliokombolewa tena na vikosi hivyo kutoka mikononi mwa UrusiPicha: Gleb Garanich/REUTERS

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, zimeiunga mkono kwa dhati Ukraine tangu Urusi ilipoivamia mwezi Februari kwa kuiwekea vikwazo chungunzima vya kiuchumi.

Kadhalika, mataifa mengi ya Magharibi yameipa Ukraine msaada wa silaha za kisasa ambazo kwa kiasi kikubwa, zimewasaidia wanajeshi wa Ukraine kuyakomboa tena maeneo ambayo awali yalikuwa mikononi mwa Urusi.

Soma pia:Urusi yatangaza kuondoa majeshi yake katika eneo la Kharkiv 

Ukraine na washirika wake wamejawa na matumaini kutokana na mafanikio ya jeshi la nchi hiyo katika eneo la mashariki la Kharkiv linalopakana na Urusi, huku Zelensky akijipiga kifua kwa kusema ushindi wa Ukraine unanukia wakati alipoutembelea mji muhimu wa Izyum, uliorudishwa mikononi mwa Ukraine wiki hii.

Scholz amrai Putin kutafuta suluhisho la kidiplomasia

Jeshi la Ukraine linaripotiwa pia kupiga hatua, japo kwa mwendo wa kobe, katika eneo la kusini la Kherson karibu na Bahari Nyeusi.

Ofisi ya rais wa Ukraine imesema leo kuwa mapigano makali yanaendelea karibu na eneo la kusini na kwamba hali ya kijeshi huko imeelezwa "kuwa ngumu sana".