Vladimir Putin arejea Kremlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Vladimir Putin arejea Kremlin

Vladimir Putin wa Urusi anarudi kwenye ikulu ya Kremlin, lakini bila ya shaka ni Warusi wachache wanaoamini kwamba kweli aliwahi kuondoka kwenye ofisi hiyo kuu.

Rais Vladimir Putin wa Urusi

Rais Vladimir Putin wa Urusi

Mwanasiasa huyu mwenye nguvu kubwa kabisa nchini Urusi alipata ushindi wa asilimia 63.6 katika uchaguzi wa tarehe 4 Machi, na mara baada ya kuapishwa hapo Jumatatu, atakuwa mtu wa kwanza kuchaguliwa mara tatu kuwa kiongozi wa taifa hilo kubwa kabisa ulimwenguni, japo sio mfululizo.

Wakati wa kampeni yake, alisema wazi kile ambacho Warusi wangelikipata kama wangelimpigia kura: "Muendelezo!" Putin alisema: "Kuna kazi kubwa iliyobakia kufanywa. Si wakati wa kusimama."

Ikulu ya Kremlin iliyopo Moscow

Ikulu ya Kremlin iliyopo Moscow

Mshirika wa kisiasa na wengine wanayemchukulia kuwa ni pandikizi la Putin, Dmitry Medvedev, alitumikia muhula ambao ulikuja kuonekana kama cha mpito kutoka mwaka 2008 hadi 2012, kabla ya mwenyewe kukataa kupigania muhula wa pili. Wachunguzi wengi wa nchi za magharibi wanaona kuwa kipindi cha Medvedev madarakani kilikuwa ni kama kuziba viraka tu.

Nafasi ya Putin kama muamuzi wa mwisho nchini Urusi, hata alipokuwa waziri mkuu chini ya Medvedev haijawahi kupingika tangu alipoingia kwenye uraisi kwa mara ya kwanza mwaka 1999.

Katika sera za nje, Putin amepigania kuendelea kwa mahusiano ya kiuchumi kati ya nchi yake na China, Urusi kuwa na uzito zaidi katika maamuzi ya kimataifa kuhusu Mashariki ya Kati na Asia ya Kati, na kampeni ya kuimarisha mahitaji ya Ulaya kwa nishati ya Urusi.

Akiwa jasusi wa zamani wa shirika la ujasusi la Urusi, KGB, amerejelea mara kadhaa kuwa Vita Baridi ni historia. Lakini wakati huu amekuwa akipigania kuijenga upya kijeshi Urusi na kuupa changamoto uwezo mkubwa wa kijeshi wa Marekani duniani.

Putin anapenda matumizi makubwa

Gari la Urusi la kubebea makombora

Gari la Urusi la kubebea makombora

Miongoni mwa silaha mpya za Urusi ambazo Putin ameziita muhimu kwa usalama wa taifa ni ndege za kijeshi zinazofanana na zile za Marekani za F-22 Raptor na mpango wa ujenzi wa nyambizi kwa ajili ya boti ya mashambulizi mara moja kila miezi 18.

Kifedha Putin ni mtetezi wa matumizi makubwa. Ameipongeza nchi yake kuwa kuwa kwenye biashara isiyo rasmi na utajiri mkubwa wa fedha za kigeni unaofikia dola bilioni 90 kwa sasa. Fedha hizo zinaweza kufika mbali katika kuondoa utegemezi wa kupindukia wa Urusi kwa mapato yatokanayo na mauzo ya nishati na usafirishaji wa malighafi, hasa kama ziwekezwa kwenye miradi ya miundombinu, amesema Putin.

Wakosoaji wa Putin nchini mwake walitabiri kwamba kutakuwa na mabadiliko machache sana ya kweli kwenye ufisadi ulioigubika nchi hiyo na dola itaendelea na kampeni yake ya kuvitenga vyombo huru vya habari na upinzani kwa utawala wa chama chake cha United Russia.

Kampeni ya kuuakandamiza uasi wa Waislamu katika maeneo ya Caucasus, unaoendelea sasa kwa miongo miwili, utaendelea huku kukiwa na uvamizi zaidi wa kijeshi na kamatamakata vya ovyo kwa wanaoshukiwa kuwa waasi, ambako nako kutaendana na uripuaji wa mabomu na mashambulizi ya waasi hao.

Wapinzani wasema Putin alilia machozi ya mamba

Lakini labda changamoto ngumu zaidi kwa awamu nyengine ya uraisi wa Putin itakuwa ni kuongezeka kwa hali ya kutokuridhika waliyonayo vijana na wasomi katika miji mikuu ya Urusi, ambao kwa siku za karibuni wameonekana kujikita zaidi kwenye matumizi ya mitandao ya intaneti kuelezea kuchoshwa kwao na urasimu, ubadhirifu wa fedha za walipa kodi na utanuaji wa misuli wa Kremlin.

Maandamano wakati wa uchaguzi wa Urusi

Maandamano wakati wa uchaguzi wa Urusi

Mwezi Disemba ulishuhudia maandamano makubwa kabisa kuwahi kufanyika katika miaka ya hivi karibuni dhidi ya serikali. Watu wenye hasira waliandamana dhidi ya wizi na udanganyifu katika uchaguzi wa bunge ambao ulikipa chama cha Yedinaya Rusiya cha Putin viti vingi. Udanganyifu wa kura ulikuwa wa wazi na mkubwa sana kiasi ya kwamba picha za vidio za maafisa wa uchaguzi wakizijaza kura walizozipiga wenyewe kwenye masanduku zilienea mitandaoni.

Katika kampeni zake za mwezi huo, Putin alisema yuko “Tayari kuondoka ikiwa Urusi haimuungi mkono.“ Televisheni ya taifa ilimuonesha kiongozi huyo akitokwa na machozi katika hotuba yake ya ushindi ya mwezi Machi.

Kwenye hotuba hiyo alisema: “Tutafanya kazi kwa uaminifu na umakini na tutafanikiwa tu.“ Baadaye Putin aliwaambia waandishi wa habari kwamba hakuwa akilia, bali ilikuwa baridi iliyorowesha macho yake. Wapinzani wake waliyaita hayo machozi ya mamba.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com