1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

vitendo vya ubakaji vyaongezeka nchini Ivory Coast.

Hafidh Kassim9 Oktoba 2006

Kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji nchini Ivory Coast kumechochea mashirika ya kutetea haki za binaadamu kutoa mwito wa kumalizwa tabia ya kuacha kuwachukulia hatua wale wanaofanya makosa haya.

https://p.dw.com/p/CHmR

Tangu mwezi September mwaka 2002, Cote d’Ivoire imegawika katika makundi mawili, ambapo upande wa kaskazini unashikiliwa na waasi na upande wa kusini unashikiliwa na serikali.

Mashirika mengi ya kutetea haki za kibinaadamu yasiyo ya kiserikali, yameripoti huvunjwa kwa mara kadhaa haki za kibinaadamu, hususan kwa wanawake na waathirika wengi katika matukio hayo huwalalamikia wanajeshi kuwa ndio wanaohusika na ubakaji.

Wakati mahakama kuu nchini Ivory Coast imepanga adhabu ya miaka 20 jela kwa yeyote atakae husika na kesi ya ubakaji, lakini machafuko ya kisiasa katika nchi hii ya Afrika Magharibi imefanya kuharibika kwa mifumo yake ya kamahakama na kupelekea kutochukuliwa hatua kwa wale wanaofanya makosa.

Mwana mama Ethel Higonnet, mtetezi na mwanaharakati kutoka katika shirika la kutetea haki za kibinaadamu lenye makao yake makuu mjini New York ambae amefanyia uchunguzi matukio ya ubakaji yanayofanyika nchini Ivory Coast kuanzia mwaka 2002, amesema kuwa nchi hiyo inaongezeka kila siku utumwa wa kimapenzi, kujamiiana na ubakaji kwa kiasi cha asilimia 70 ya wanawake nchini Ivory Coast wakidhalilishwa kijinsia.

„Huko magharibi hali ni ya machafuko. Hakuna kijiji hata kimoja ambacho mwanamke hajawahi kujafanywa mtumwa wa mapenzi. Kuna matukio ya ubakaji kila wiki katika kata zote“. Alisema Ethel Higonnet wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari katika mji wa kibiashara wa nchi hiyo Abijan ambako aliwasilisha uchunguzi wake.

Bibi Higonnet vile vile aliongeza kuwa umri wa wale wanaofanyiwa vitendo hivyo ni kuanzia miaka mitatu hadi 75.

Aidha mtetezi huyo wa haki za binaadamu amesema kwa kipindi cha miaka minne shirika lake limeona kesi tatu tu za ubakaji zilizotolewa hukumu ya adhabu huko magharibi mwa nchi, jambo ambalo ni lakutisha.

Amesema huku kusini mwa Ivory Coast, vituo vya uangalizi vya kijeshi vimekuwa ni kitovu cha matukio ya ubakaji ambako wanajeshi huwabaka vujana wa kike.

Bibi Tenin Toure-Diabate, Profesa wa masuala ya Jamii katika chuo kikuu cha cocody mjini Abijana, anaamini kuwa ni muhimu kwa makamanda wa kijeshi kuwa na kipimo cha nidhamu katika vikosi vyao ili kusimamisha vitendo vya ubakaji kwa wanawake.

„Bila ya hili, mapendekezo yote na michango ya maana itakuwa ni bure“ Bibi Tenin Toure-Diabate aliliambia shirika la habari la IPS, kauli ambayo ilikuwa ni sawa na ile iliyotolewa na bibi Higonnet kuhusu kuwekwa sheria madhubuti juu vyombo vya usalama kuhusu suala la ubakaji.

Bibi Higonnet pia amevilaumu vituo vya matibabu vya nchini Ivory Coast kwa kushindwa kutoa msaada kwa waathirika ili sheria ifuate mkondo wake, ikitiliwa maanani jinsi wanawake wanavyoathirika na magonjwa kadhaa baada ya kubakwa kama maambukizi ya Ukimwi na kadhalika.