Vitendo vya kihalifu vyaongezeka Haiti | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.01.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Vitendo vya kihalifu vyaongezeka Haiti

Uhalifu unaongezeka kufuatia wafungwa katika gereza kuu kutoroka usiku ambao tetemeko la ardhi lilitokea

Rais wa zamani wa Marekani na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Bill Clinton.

Rais wa zamani wa Marekani na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Bill Clinton.

Maafisa wameonya kuwa mazingira magumu yaliyotokana na tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Haiti yameongeza hali ya wasi wasi nchini humo kufuatia kukithiri kwa vitendo vya kihalifu, ikiwemo ubakaji wa wanawake katika kambi kadhaa na kuzuka kwa vurugu wakati wa utoaji misaada ya kibinaadamu kutoka katika mashirika mbalimbali ya misaada.

Pamoja na kuendelezwa jitihada ya utoaji wa misaada ya kimataifa baada ya kutokea kwa tetemeko hilo la ardhi tarehe 12 ya mwezi huu, mamia ya maelfu ya watu wasio na makaazi ambao wanaishi katika kambi mbalimbali siyo tu wanakabiliwa na uhaba wa chakula, bali pia wako katika hatari ya kuongezeka vitendo vya kihalifu. Mariana Merise, mwenye umri wa miaka 40, anayeishi katika kambi moja iliyopo kwenye Ikulu ya nchi hiyo ambayo pia iliathiriwa na tetemeko hilo la ardhi, amesema ni Yesu Kristo tu ndio anawalinda, kwani watu wanaoishi katika eneo hilo wamekuwa wakibugudhiwa na makundi ya wahuni na wahalifu ambao wanawaibia vitu vyao. Mkuu wa polisi nchini Haiti, Mario Andresol, amesema kwa sababu ya kukosekana umeme katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince, majangili wanatumia nafasi hiyo kuwasumbua na kuwabaka wanawake na wasichana wadogo katika kambi hizo.

Andresol anasema maelfu ya wafungwa waliotoroka katika gereza kuu usiku ambao nchi hiyo ilikumbwa na tetemeko la ardhi lililokuwa na kipimo cha Richter cha 7.0. wamegeuka mbwa mwitu na kikosi cha polisi kinazidisha nguvu kutokana na askari polisi wengi kuuawa kutokana na tetemeko hilo ambapo wengine bado hawajulikani walipo. Makamu wa mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Anthony Banbury, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa watu waliosalimika na tetemeko hilo la ardhi wanasimama katika misururu mirefu kugonjea kupatiwa misaada ambapo mara nyingine vurugu hutokea.

Shule kufunguliwa Jumatatu ijayo

Katika hatua nyingine, wizara ya elimu nchini Haiti imeeleza kuwa shule katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ambazo hazikuathiriwa sana na tetemeko la ardhi, zitafunguliwa Jumatatu ijayo na maafisa wanafanya jitihada za kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea shuleni. Maafisa wa elimu nchini humo na mashirika ya misaada yataanza kufanya tathmini ya shule za serikali na binafsi katika mji mkuu wa Port-au-Prince na miji mingine iliyoathiriwa vibaya na tetemeko hilo la ardhi. Tetemeko la ardhi lililotokea nchini Haiti limesababisha vifo vya watu 200,000. Maafisa wa elimu na mashirika ya misaada yamesema kiasi watoto milioni 1.8 wameathiriwa na tetemeko hilo huku kati ya shule 5,000 hadi 8,000 zikiwa nazo zimeathiriwa pia.

Wito kwa jumuiya ya kimataifa

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Bill Clinton, akizungumza katika kongamano la kiuchumi duniani mjini Davos, Uswisi, aliwataka viongozi wa kisiasa na kibiashara duniani kuisaidia Haiti. Umoja wa Mataifa umesema kuwa ahadi ya misaada ya kimataifa na ufadhili uliotolewa jana Alhamisi kwa ajili ya Haiti imefikia dola bilioni mbili, lakini jukumu la kuifanya nchi hiyo kujisimamia yenyewe bado ni kubwa. Makamu wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, Paul Farmer, amesema zaidi ya robo tatu ya mji mkuu wa Port-au-Prince umeharibiwa vibaya na utahitaji kujengwa upya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 29.01.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LmeL
 • Tarehe 29.01.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LmeL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com