1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyanyemelea Sudan Kusini

23 Desemba 2013

Jeshi la Sudan Kusini limesema linajiandaa kufanya shambulio kubwa dhidi ya vikosi vya waasi wakati nchi hiyo ikielekea kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe licha ya juhudi za kimataifa za kutafuta amani.

https://p.dw.com/p/1Af3u
Wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini.
Wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini.Picha: Adriane Ohanesian/AFP/Getty Images

Uwezekano wa kuzuka kwa mapigano makubwa umekuja wakati Umoja wa Mataifa ikionya kwamba hali katika taifa hilo jipya hilo changa kabisa duniani inatibuka kwa haraka ambapo hivi sasa mamia kwa maelfu ya raia wakiwa katika hatari.Inaripotiwa kwamba idadi ya vifo kutokana na machafuko ya umwagaji damu ya wiki iliopita inaweza kupindukia 1,000.

Mapigano yameikumba Sudan Kusini kwa zaidi ya wiki moja baada ya Rais Salva Kiir kumshutumu makamo wake Riek Machar kufanya jaribio la mapinduzi baada ya kumtimuwa kutoka serikalini hapo mwezi wa Julai.

Machar amekanusha madai hayo na kumshutumu Kiir kwa kwa kuchukuwa hatua kali ya kuwaadhibu wapinzani wake. Machar ameapa kumuondowa Kiir madarakani na vikosi vyake tayari vimeuteka mji wa Bor ambao ni mji mkuu wa jimbo lenye vurugu la Jonglei ukiwa kama kilomita 200 tu kaskazini mwa mji mkuu wa Juba na pia wameuteka mji wa Bentiu ambao ni mji mkuu wa jimbo muhimu lenye kuzalisha mafuta la Unity.

Mwanajeshi wa kabila la Lou Nuer la aliyekuwa Makamo wa Rais wa Sudan Kusini aliyetimuliwa Riek Machar.
Mwanajeshi wa kabila la Lou Nuer la aliyekuwa Makamo wa Rais wa Sudan Kusini aliyetimuliwa Riek Machar.Picha: Camille Lepage/AFP/Getty Images

Serikali yajiandaa kwa mashambulizi

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer amesema serikali imechukuwa hatua ya kufanya mashambulizi.

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi wao wataukombowa mji mwa Bor kutoka kwa vikosi vya waasi na kwamba mji huo bado unadhibitiwa na vikosi vya Machar lakini wanajiandaa kuudhibiti tena mji huo.

Matamshi hayo yanakuja licha ya kuwepo kwa juhudi za kidiplomasia za mataifa ya Afrika na wito kutoka Marekani,Uingereza na Umoja wa Mataifa wa kutaka kusitishwa kwa mapigano hayo.

Mratibu mkuu wa masuala ya misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Toby Lanzer ameutembelea mji huo wa Bor hapo jana na kusema kwamba hali inazidi kuwa mbaya. Amesema kuna maelfu ya raia wa Sudan Kusini waliokimbilia vichakani au kurudi kwenye vijiji vyao ili kuepuka madhara.

Vita vyanyemelea Bor

Ameongeza kusema ana wasi wasi mkubwa wa vita vinavyounyemelea mji huo ambapo amekiri kwamba ni jambo lisiloyumkinika kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kuwa katika uwezo wa kuwalinda raia wanaokadiriwa kufikia 15,000 wanaotafuta hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa ilioko huko.Kwa mujibu wa Lanzer raia wa Australia,Uganda na Ethiopia ni miongoni mwa watu hao waliotafuta hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa huko Bor.

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa pia amesema helikopta za kiraia zimewahamisha raia wa Marekani kutoka mji huo ulioshuhudia mashambulizi mazito ya bunduki za rashasha lakini kuna raia 3,000 wa nchi kama vile Canada,Uingereza na Kenya wanaoendelea kukwama katika mji huo.

Wakimbizi waliokimbilia kujihifadhi kwenye kambi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa huko Bor.(18.12.2013).
Wakimbizi waliokimbilia kujihifadhi kwenye kambi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa huko Bor.(18.12.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Lanzer ambaye anatafuta msaada wa kifedha wa haraka kutoka Jumuiya ya Kimataifa amesema idadi ya wakimbizi wa ndani ya nchi inaweza kupindukia 100,000.

Rais Barack Obama wa Marekani mwishoni mwa juma ametuma baruwa kwa viongozi wa bunge la nchi hiyo akiwajulisha kwamba huenda akachukuwa hatua zaidi za kijeshi Sudan Kusini ili kuwalinda raia wa Marekani, wafanyakazi na mali zao.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri:Yusuf Saumu