1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Obama dhidi ya Al-Qaeda

8 Januari 2010

Tangu lilipotokea jaribio la kutaka kuiripua ndege ya Marekani tarehe 25 Desemba, Rais wa Marekani Barack Obama kwa mara ya tatu amezungumzia rasmi suali hilo.

https://p.dw.com/p/LOYk
President Barack Obama speaks in the State Dining Room of the White House in Washington, Thursday, Jan. 7, 2010, about an alleged terrorist attempt to destroy a Detroit-bound U.S. airliner. (AP Photo/Charles Dharapak)
Rais wa Marekani,Barack Obama.Picha: AP

Siku ya Alkhamisi Obama alisema kuwa yeye anachukua jukumu la kosa la kutogundua mapema mpango uliohusika na jaribio hilo na aliongezea kuwa tukio hilo wala si kosa la mtu bali mfumo wa usalama ndio ulio na dosari.

Rais huyo wa marekani ametoa amri ya kuchukuliwa hatua mbali mbali katika sekta zote zinazohusika na usalama wa taifa. Kwanza kabisa ukaguzi wa abiria uwe mkali zaidi kwenye viwanja vya ndege na vile vile ihakikishwe kuwa idara za upelelezi zitafuatiliza kikamilifu panapozuka mashaka yo yote. Katika hotuba yake Obama alieleza waziwazi kuwa Marekani ipo vitani, lakini vita hivyo si dhidi ya adui wa mawazo bali adui huyo ana jina. Alisema:

"Tupo vitani dhidi ya Al Qaeda, mtandao uliojaa chuki na unaotumia nguvu- mtandao uliotushambulia Septemba 11 na uliouwa takriban watu 3,000 wasio na hatia na unaopanga kutushambulia tena."

Obama akaeleza kuwa serikali yake itafanya kila iwezalo kumshinda adui huyo. Hiyo ni kinyume kabisa na vile alivyokosa makamu wa zamani wa rais, Dick Cheney.Mwanachama huyo wa Republikan alisema Obama atakuwa akiiongoza Marekani kama nchi isiyo vitani. Alionya kuwa hali ya usalama kwa hivyo itadhoofika kuliko ilivyokuwa wakati wa utawala wa Bush.

Lakini mtaalamu wa masuala ya usalama wa taifa,Ken Gude wa Kituo cha maendeleo ya Wamarekani mjini Washington anasema, yaonekana kana kwamba msimamo wa Obama si mkali kama wa mtangulizi wake. Gude anasema ukweli wa mambo ni kwamba serikali ya Obama inachukua hatua kali kupambana na ugaidi na hasa dhidi ya Al Qaeda. Kwa mfano, mashambulio yanayofanywa na ndege zisizo na rubani yameongezeka nchini Pakistan. Vile vile serikali ya Yemen inapata msaada zaidi kupiga vita ugaidi. Hata idadi ya wanajeshi wa Marekani wanaopigana dhidi ya Al Qaeda nchini Afghanistan itaongezwa kwa mara tatu chini ya utawala wa Obama

Hata hivyo,jaribio la shambulio lililozuiliwa siku ya Krismasi, limedhihirisha kuwa idara za upelelezi za Marekani zilidharau uwezo wa maadui wake. Hawakutambua jinsi kundi la Al Qaeda linavyohatarisha Rasi ya Uarabuni. Mshauri wa Obama kuhusu masuala ya usalama John Brennan amegundua dosari hiyo.Anasema wao waliamini kuwa lengo la muda mrefu la Al Qaeda, ni kuishambulia Marekani lakini, hawakujua kuwa kundi hilo lilikuwa tayari kutekeleza mpango wake. Sasa lakini wamegutuka na wamekuwa wajanja na hatua zinazohitajika zitachukuliwa.

Mwandishi: Bergmann,Christina/ZPR/P.Martin

Mhariri:Othman,Miraji