Vita vya Gaza Magazetini | Magazetini | DW | 21.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Vita vya Gaza Magazetini

Vita vya Gaza,na kudunguliwa ndege ya abiria ya Malaysia katika anga la Ukraine ndizo mada zilizohodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani .

Mizinga ya Israel yavurumishwa katika mji wa Shuhaia,huko Gaza

Mizinga ya Israel yavurumishwa katika mji wa Shuhaia,huko Gaza

Tuanzie Mashariki ya kati ambako hujuma tangu za hewani mpaka za nchi kavu za Israel zimeshaangamiza maisha ya zaidi ya wapalastina mia tano na waisrael 20 na mmoja kutekwa nyara na Ezzudine el Kasim-tawi la kijeshi la Hamas.Frankfurter Allgemeine linajiuliza vita vitamalizika lini?:" Damu inazidi kumwagika kila kukicha. Picha za kuhuzunisha na zinazotisha zinaonyeshwa katika kila pembe ya dunia. Lakini mwisho wa vita hakuna anaeweza kuukadiria.Na ni jambo la kutegemea, hata vita hivi vya sasa vikimalizika,Hamas hawatadhoofika,sawa na ilivyokuwa katika vita vilivyopita.Kwasababu baada ya kila vita mshikamano miongoni mwa wapalastina unakuwa mkubwa na wa dhati seuze madai ya Hamas hayakutiwa chunvi na wala si jambo lisilowezekana . Hamas wanadai hatua za kuizingira Gaza zipunguzwe makali ili kurahisisha hatimae shughuli za kiuchumi. Bila ya kuwa na matumaini wapalastina wanaoishi katika ukanda wa Gaza,amani haitapatikana.Na pekee mashambulio ya nchi kavu hayatasaidia kuwazuwia Hamas wasifyetue makombora dhidi ya Israel.

Matarajio yawekewa juhudi za kidemplomasia

Hannoversche Allgemeine linataraji juhudi za kidiplomasia zitaleta tija.Gazeti linaendelea kuandika:"Netanyahu anaweza kujipiga kifua kwamba kansela Angela Merkel na rais Barack Obama wanazungumzia juu ya haki ya Irael ya kujihami. Lakini Netanyahu anakosea anapotaka kuigeuza kauli hiyo kuwa "idhini" ya kuzidi kuhujumu eneo lote la kilomita 40 la Ukanda wa Gaza.Kila picha ya watoto wa kipalastina waliouwawa sio tu ni laana kwa yanayofanywa na Israel bali pia kwa nchi za magharibi. Kilichosalia ni kutaraji tu kwamba waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry atafanikiwa kuitanabahisha Israel atakapoanza ziara yake katika eneo hilo.

Putin ajitoe bila ya aibu katika mzozo wa Ukraine

Prorussische Separatisten

Wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi wakilizunguka eneo ndege ya abiria ya Malaysia ilipoangukia Karibu na Donetsk

Kisa cha kudunguliwa ndege ya abiria MH 017 ya Malaysia kinazidi kuwashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani.Schwäbishe Zeitung linatathmini uwezekano wa kutumwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa nchini Ukraine.Gazeti linaendelea kuandika:" Ulaya na Ujerumani hazikufanya vya kutosha katika mzozo wa Ukraine. Hiyo ndiyo hoja anayoitumia mbunge wa Ravensburger Andreas Schockenhoff.Madai yake kutaka vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa vipelekwe,kijuu juu mtu anaweza kusema hayana uzito au ameotea. Lakini ukichunguza kwa dhati utagundua hajakosea. Urusi na rais Putin wanazidi kukabwa na shinikizo la kimataifa kwa mchango wao usiokadirika mashariki ya Ukraine. Kukubaliwa mpango wa kutumwa wanajeshi wa kulinda amani Ukraine itakuwa njia mojawapo kwa Putin kujitoa bila ya aibu katika janga alimotumbukia baada ya kudunguliwa ndege ya abiria ya Malaysia chapa MH 017.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandsperrse

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman