Visa vya Trump vyagonga vichwa vya magazeti Ujerumani | Magazetini | DW | 31.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Visa vya Trump vyagonga vichwa vya magazeti Ujerumani

Vishindo vya rais mpya wa Marekani Donald Trump na shambulio la kisu mjini Hamburg ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani.

Tunaanzia Marekani ambako rais Trump haipiti siku kabla ya kugonga vichwa vya habari. Utawala wake unatajwa kuwa "vurugu". Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:"Yadhihirika kana kwamba mwenyewe Trump, anaejinata kuwa rais bora kuliko wote, ameshagundua, hakuna kinachoendelea: Mtu anaweza kusema: mhula wake madarakani mpaka sasa ni vurugu tupu na sio tu kwa mtazamo wa wale wanaohisi hakustahili kuwa rais. Hata katika chama chake mwenyewe ameondolewa patupu katika sera ya mageuzi ya huduma za afya, Obamacare, imani ya wananchi kwake imepungua na ikulu ya Marekani White House imegeuka uwanja wa mapambano kati ya makundi yanayohasimiana."

Trump aonyesha misuli katika mvutano na Korea ya Kaskazini

Licha ya kuchujuka sifa yake nchini maji yanaonyesha kuzidi unga katika mvutano pamoja na Korea ya Kaskazini. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika: "Mzozo pamoja na Korea ya Kaskazini unazidi kupamba moto. Washington imetoa jibu kali dhidi ya jaribio la hivi karibuni la kombora la kinuklea la Korea ya Kaskazini linalotajikana kuwa na uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 1000 au zaidi , kwa maneno mengine uwezo wa kupiga kokote kule nchini Marekani. Yadhihirika kana kwamba Washington inataka kuwatunishia misuli yake viongozi wa mjini Pyongyang  na pia watetezi wao, viongozi wa China: mpaka ndio huo , wasiuvuke."

 

Shambulio la kisu mjini Hamburg

Nchini Ujerumani wahariri wamemulika na visa vya mashambulio ya mara kwa mara yanayofanywa kwa sehemu kubwa na vijana wanaoomba kinga ya ukimbizi. La hivi karibuni kabisa limetokea katika mji wa kaskazini wa Hamburg. Limefanywa na kijana wa miaka 26 mwenye asili ya Palastina aliyezaliwa katika falme za nchi za kiarabu na ambae maombi yake ya ukimbizi yamekataliwa nchini Ujerumani. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika: "Baada ya shambulio hilo la Hamburg baadhi ya wanasiasa wanahimiza hatua kali zichukuliwe. Lakini saa 24 hazijakamilika tangu shambulio hilo kutokea na kuanza kufanya kazi sheria kali zaidi kuhusu kurejeshwa makwao wakimbizi waliokataliwa kinga ya ukimbizi.

Tatizo ni lile lile: sheria zikipitishwa zinabidi pia zitumike. Panahitajika kwa hivyo ushirikiano bora zaidi kati ya idara za usalama. Kadhia ya kijana huyu wa kipalastina inafichua tatizo jengine lililoko katika upande wa usalama. Alikuwa peke yake na  shamabulio lake  hakulipanga kabla. Hata silaha aliyoitumia hakuja nayo, ameiiba katika duka kuu hilo hilo alikofanya shambulio hilo. Nafasi ya kuzuwia shambulio kama hilo ni ndogo sana. Lakini huenda ilikuwa bahati nzuri, kwamba muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu, walikuwa vijana chungu nzima wenye asili ya Afghanistan, Uturuki na Tunisia waliomfuata mbio kijana huyo na kumkamata kabla ya polisi kufika. Wanastahiki sifa, na wao ndio mashujaa wa Barmbek."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com