1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Virusi vya madeni vyaenea kanda ya euro

24 Novemba 2011

Mvutano unaoendelea kuhusu mzozo wa madeni katika kanda ya Euro, bajeti ya Ujerumani na usafirishaji wa taka za nyuklia ni baadhi ya mada zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani, Alkhamisi ya leo.

https://p.dw.com/p/RyGA

Basi tutaanza na gazeti la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linaloandika kuhusu mdahalo unaoendelea katika bunge la Ujerumani mjini Berlin juu ya bajeti ya mwakani. Linasema:

"Serikali imekosa kukitumia kipindi hiki cha neema kujiandaa kwa mustakabali wa taifa. Na upande wa upinzani ulikuwa na haki ya kuikosoa bajeti iliyopendekezwa. Lakini Kansela Angela Merkel wala hakushughulishwa na lawama zilizotolewa. Lakini hali hiyo inaweza kubadilika haraka, hasa kwa kuzingatia kile kilichotokea hapo jana, baada ya masoko ya hisa kupoteza imani katika dhamana za serikali ya Ujerumani. Hata Ujerumani, huenda ikalazimika kulipa riba kubwa zaidi kwa mikopo yake. Kilichotokea katika masoko ya hisa kitaathiri bajeti iliyopendekezwa bungeni hapo jana."

Gazeti la BADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN limeshughulikia mzozo wa madeni katika kanda inayotumia sarafu ya euro. Linasema:

"Njia bado ni ndefu kabla ya utulivu kuweza kupatikana katika Umoja wa Ulaya, kwani nchi wanachama zitapaswa kuachia sehemu kubwa ya mamlaka yao ya kitaifa kuliko vile ilivyotazamiwa. Tatizo ni kuwa ili kuweza kufanya hivyo, katiba ya Umoja wa Ulaya itapaswa kubadilishwa na hatua hiyo itahitaji muda - muda ambao waokozi wa sarafu ya euro hawana. Kwani kwa haraka wanapaswa kuwa na mpango wa kuuzuia mzozo wa madeni kuenea katika kanda nzima ya euro."

Gazeti la TAGESSPIEGEL likiendelea na mada hiyo hiyo linaandika:

"Umoja wa Ulaya na Ujerumani zinatofauti zake na hiyo ni ishara mbaya katika wakati huu wa mzozo.Tangu miaka miwili umoja huo unapambana na mzozo wa madeni katika kanda ya euro na ionekanavyo viongozi hawakujifunza lo lote. Wakati Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso akipendekeza kuwa na dhamana za umoja huo, kuzisaidia nchi zenye madeni katika kanda ya euro, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaendelea kuipinga fikra hiyo. Virusi vya madeni vinaenea barani Ulaya - hatari ya kuambukizwa inazidi kuwa kubwa."

Kwa kumalizia tunageukia mada nyingine - usafirishaji wa taka za nyuklia za Ujerumani. Gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE linaonya kuwa wiki inayokuja, itashuhudia wapinzani wa nishati ya nyuklia wakiziba njia za reli huku wakijaribu kuwakwepa polisi na wengine watakuwa wakiandamana. Hatimae kutakuwepo majeruhi na wengi wengine, watakamatwa. Na yote hayo, yataigharimu serikali, mamilioni ya euro. Kwa kweli safari hii usafirishaji wa taka hizo za nyuklia ungeenda vingine, kwani serikali imeshamua kuachana na matumizi ya nishati ya nyuklia hatimae na hilo ndio lililokuwa likidaiwa na vuguvugu la wapinzani wa nishati ya nyuklia.

Mwandishi:Prema Martin/dpa

Mhariri: M.Abdul-Rahman