Vipi Ugiriki kujikomboa na madeni yake ? | Magazetini | DW | 06.05.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Vipi Ugiriki kujikomboa na madeni yake ?

Vipi Ujerumani ishirikiane ?

default

Waziri-mkuu George Papandreou anakunywa maji kukata kiu cha madeni ?

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo, yametuwama tena juu ya msukosuko wa madeni ya Ugiriki na jinsi, unavyoathiri sarafu ya Euro.Wahariri wengine lakini, wamezungumzia mkataba wa kutoeneza silaha za nuklia na hukumu aliyopitishiwa Bw.Schreiber, alierudishwa Ujerumani kutoka Kanada, kukabili mashtaka ya kukwepa kulipa kodi kutoka marupurupu aliyojipatia kwa biashara ya silaha.

FLENSBURGER TAGEBLATT juu ya mzozo wa madeni wa Ugiriki na hatua za kuikomboa isifiliske: Laandika:

"Katika Tangazo lake la serikali Bungeni (Bundestag), Kanzela Angela Merkel, alitumia maneno makubwa:Lakini, katika matamshi yake hayo, hakuchukua hata hatua moja kuuridhia Upinzani.Hakutoa mualiko wa kushaurina nao huko Ikulu,wala hakuwanon'goneza faraghani nini kinapita.

Badala ya kujenga jukwaa pana la maridhiano na vyama mbali mbali,anataka sasa idhini yao kutoa mkopo wa mabilioni , unaoharakishwa kupitishwa bungeni.Haraka hizo za nini ? Kwani, msukosuko wa Ugiriki , haukuibuka leo .Ni serikali ya Ujerumani, iliolala usingizi."

Laandika Flensburger Tageblatt.

Ama gazeti la REUTLINGER-GENERAL-ANZEIGER linahisi kwamba, Kanzela Merkel aliepitisha muda mrefu akinyatia , jana alitumia maneno makali:

"Ni hatima ya ulaya hapa ilio hatarini. Upinzani katika Bunge mjini Berlin , unadai tena kwa haki, sio tu usaidie kifedha,bali pia katika kutunga sheria za kimataifa za kupambana na biashara ya walanguzi."

BADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN, linamgeukia waziri mkuu Papandreou wa Ugiriki .Linaandika kwamba, kwa jicho la wimbi la machafuko mjini Athen, hali yake inazidi kuwa ya kutatanisha kuweza kupitisha binafsi sheria anazopanga kuzipitisha .

Kwa mfano, laandika gazeti:

"Kupandisha kodi ya mauzo ,kungefanikishwa endapo kutokana na ukaguzi mkali zaidi, ingefahamika iwapo kweli kodi zinalipwa na wote.Ni pale Ugiriki ikiachana na mchezo wa kukwepa kulipa kodi za mapato, ndipo itapoweza kukusanya fedha za kutosha ili kujaza mfuko wa hazina yake iweze siku moja kulipa madeni ya washirika wake wa Umoja wa Ulaya."

Ama kuhusu mashtaka yaliomkabili Bw. Schreiber, kuna dhana- lasema gazeti la LAUSITZER RUNDSCHAU kwamba, hatia kubwa ya kukwepa kodi imegubikwa hapa na kiza juu ya kashfa ya michango ya siri .Hii inatokana na sababu moja: Laandika gazeti:

"Ahadi aliotoa Schreiber ya kuanika hadharani, dhahiri-shahiri kashfa kubwa ,imedhihirika ni kelele tupu.Kinachovunja moyo zaidi, ni matokeo ya kesi hii kwa lengo la kusafisha siasa za nchi hii.Kwani, kuna waliotaka sana kujua Bw.Schreiber, kwa kukihonga fedha chama cha CDU, alitaka nini na nani , katika chama cha CDU alipokea fedha hizo."

Mwandishi:Ramadhan Ali /Dt Agenturen

Mpitiaji:Moahammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com