Viongozi wajadili usalama wa dunia Munich | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wajadili usalama wa dunia Munich

Katika siku ya kwanza ya mkutano wa usalama wa Munich umeibua maswali magumu kuhusu mustakabali wa Umoja wa Ulaya, mchango wa Marekani ulimwenguni na kutoweka kwa mahusiano ya kimataifa.

Bila ya kuwepo kwa majibu rahisi kuhusiana na maswali hayo, viongozi wa nchi, viongozi wa kijeshi na wabunge wanajaribu kutafuta ufumbuzi wa changamoto chungu nzima zilizojitokeza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mojawapo ya sababu za changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuchaguliwa kwa Donald Trump kuwa Rais wa Marekani na kujiondoa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya.

Lakini swali kuu ni wasiwasi kuhusu wajibu wa Marekani kama mshikadau mkuu wa misingi ya kiliberali, demokrasia na kuwa dola yenye nguvu zaidi duniani, na iwapo utawala mpya ulio madarakani nchini humo utaendeleza hayo katika nyanja ya kimataifa.

Mratibu wa mkutano huo wa usalama wa Munich balozi wa zamani wa Ujerumani nchini Marekani Wolfgang Ischinger ameieleza DW kuwa mambo huenda yasiende vizuri iwapo Marekani itaendelea kuunga mkono mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kama ya Uingereza ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis amesisitiza juu ya ahadi ya nchi hiyo ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi washirika wa Jumuiya ya kujihami ya NATO. Mattis ameuambia mkutano huo wa Munich unaowaleta pamoja viongozi wa nchi kadhaa na zaidi ya mawaziri 70 wa ulinzi kuwa Rais Trump anaunga mkono jumuiya ya NATO.

Marekani itachukua mkondo gani chini ya Trump?

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von Der Leyen amesema ni muhimu kwao kufahamu ni msimamo upi hasa Marekani inachukua na kuwa na hakika kuwa utawala mpya unaweza kuaminika kuhusu sera za kiusalama..

Münchner Sicherheitskonferenz (AFP/Getty Images)

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen

Trump amewatia wasiwasi washirika wa Marekani kutokana na uhusiano wake wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence leo Jumamosi, atahutubia mkutano huo wa usalama wa Munich unaoingia siku ya pili. Mshauri mkuu wa sera za kigeni wa Ikulu ya rais ya White House amesema Pence anatarajiwa kuihakikishia Ulaya kama mshirika imara wa Marekani.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amesema changamoto nyingi zinazoukumba Umoja wa Ulaya zimetokana na ukosefu wa ufahamu kuhusu misingi mikuu ya umoja huo. Schäuble amesema tatizo lao kuuu ni kuwa watu kote barani Ulaya hawaziamini asasi za Umoja wa Ulaya na hivyo wanahitaji kufahamu kwanini kuna haja ya utangamano wa Ulaya.

Mashirika ya kijasusi ya Ulaya yameonya kuwa Urusi inalenga kuziyumbisha serikali na kushawishi matokeo ya chaguzi barani Ulaya kwa kufanya udukuzi, kueneza taarifa zisizo sahihi, propaganda na kuvifadhili vyama vilivyo na misimamo mikali vya mrengo wa kulia.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg alifanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov katika mkutano huo wa Munich, katika kuishurutisha Urusi kuwa wazi zaidi kuhusu shughuli zake za kijeshi ambazo hazitabiriki.

Mwandishi: Caro Robi/ Reuters/Dw English

Mhariri: Isaac Gamba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com