1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya na Afrika wajadili kuhusu nishati

Josephat Charo7 Machi 2007

Mkutano wa siku mbili kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika kuhusu nishati unamalizika leo mjini Berlin hapa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHIn
Waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani Heidermarie Wieczorek-Zeul
Waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani Heidermarie Wieczorek-ZeulPicha: AP

Ulaya inahitaji nishati na Afrika inataka kuuza nishati. Inaweza kufikiriwa kwamba mabara haya mawili yanaweza kufanya biashara pamoja lakini jambo hili si rahisi. Malighafi kama vile mafuta na makaa ya mawe si baraka kila mara kwani zinaweza kuhatarisha mazingira na kusababisha ufisadi na kuporomoka kwa uchumi barani Afrika. Umoja wa Ulaya ukitaka kuzuia hayo, uliwalika viongozi wa Afrika kuhudhuria mkutano wa siku mbili mjini Berlin.

Makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini, mafuta kutoka Nigeria na gesi kutoka Angola. Katika bara la Afrika kuna karibu kila kitu kinachohitajika katika viwanda, hususan barani Ulaya ambako kuna mahitaji makubwa ya nishati lakini malighafi kidogo. Wazungu hununua mafuta, gesi na makaa ya mawe kutoka Mashariki ya Kati na Urusi, muuzaji mkubwa wa nishati wa Ulaya. Kinyume cha mambo ni kwamba Wazungu hawajawekeza sana Afrika kama anavyosema Felix Mutati, waziri wa nishati wa Zambia.

´Wazungu wamekuwa wakisema sababu kwa nini hawataki kuwekeza barani Afrika ni misukosuko ya kisiasa. Kwa hiyo kwa wakati huu wametoa mwanya kwa nchi kama China kujaza pengo waliloliacha kwa muda mrefu. Kwa hiyo unakuta China imewekeza barani Afrika na inapata nishati kutoka Afrika. Wazungu wamechelewa na wanakuja baada ya China.´

Mambo yanatarajiwa kubadilika kwani Umoja wa Ulaya unataka kushirikiana zaidi na Afrika. Ndio maana serikali ya Ujerumani imewaalika viongozi wa kiafrika kuhudhuria mkutano wa mjini Berlin kwa kuwa Ujerumani ni mweyekiti wa umoja huo. Aoumar Abdoul Dhabeh ni katibu mkuu katika wizara ya nishati nchini Chad. Nchi yake inaweza kuwa kivutio kwa Ulaya kwa sababu Chad kwa wakati huu hutoa mapipa laki mbili ya mafuta kila siku.

´Kwa muda wa miaka mitatu tumekuwa tukisisitiza matumizi ya mafuta ya ardhini ingawa sera ya sasa inatuwama sana juu ya uvumbuzi wa nishati inayoweza kufanywa upya. Hii ni kwa sababu tuna uwezo mkubwa wa kutengeza nishati kutokana na upepo na jua. Kwa hiyo nishati ya jua inatakiwa itusaidie katika kujenga mfumo mzima wa nishati.´

Chad inahitaji msaada wa Umoja wa Ulaya kwa sababu una ujuzi kuhusu nishati endelevu na unaweza kusaidia kutoa mafunzo kwa wahandisi. Linapokuja swala la nishati kutokana na upepo, Ujerumani ndio inayofaa kutoa teknolojia hiyo. Waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani, Heidermarie Wieczorek-Zeul amesema Ujerumani iko tayari kuendeleza nishati endelevu barani Afrika.

Mwaka uliopita Ujerumani ilitumia euro milioni 400 kwa miradi ya nishati barani Afrika, nusu kati yao ikiwa ya nishati endelevu. Waziri Heidermarie Wieczorek-Zeul anataka washirika wengine wajitolee zaidi.

´Hata washirika wa Umoja wa Ulaya na benki ya dunia pia wajitolee zaidi kwa dhati katika uwekezaji muhimu kwenye swala la nishati na juu ya yote katika mambo yanayoweza kusaidia hatua mbadala ambazo kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa ni muhimu.´

Heidermarie Wiezorek-Zeul amewambia wajumbe wa mkutano wa mjini Berlin kwamba bila upepo, jua na maji hakuna maendeleo endelevu yanayoweza kupatikana. Amesisitiza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kukabiliwa kutumia nishati endelevu.