Viongozi wa Sudan Kusini kuunda serikali ya mpito | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Sudan Kusini kuunda serikali ya mpito

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wamekubaliana kuunda serikali ya mpito katika kipindi cha siku sitini zijazo ili kujaribu kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemarian Desalegn ameyatangaza hayo hapo jana baada ya mkutano kati ya viongozi hao wawili mahasimu pembezoni mwa mkutano wa jumuiya ya ushirikiano wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD mjini Addis Ababa.

Haile mariam amesema Rais Kiir na aliyekuwa makamu wake Machar wamekubaliana kukamilisha mchakato wa maridhiano katika miezi miwili ijayo ambapo wataangazia jinsi gani watakavyoweza kuinda serikali hiyo ya mpito na ni nani atashirikishwa.

IGAD yatishia vikwazo

IGAD kwa mara ya kwanza kupitia kwa mwenyekiti wake ambaye n waziri huyo mkuu wa Ethiopia imetishia kuziwekea pande zote mbili zinazo zozana vikwazo na hatua nyingine kali kama hazitasitisha operesheni zote za kijeshi na zitaendelea kutatiza juhudi za kufikiwa kwa amani.

Rais Salva Kiir(kushoto) na Riek Machar(Kulia) wakipatanishwa

Rais Salva Kiir(kushoto) na Riek Machar(Kulia) wakipatanishwa

Haile Mariam amesema pande hizo mbili zimekubali kujitolea kikamilifu kuheshimu mikataba iliyotiwa saini katika kipindi cha nyuma.Matamshi ambayo yametiliwa mkazo na msemaji wa rais Kiir Ateny Wek Ateny

Mjumbe wa Marekani nchini Sudan Kusini Donald Booth amesema mazungumzo hayo ya amani yaliyoandaliwa na IGAD yanatoa fursa ya mwisho nzuri zaidi kwa pande zote mbili kuthibitisha kuwa zinanuia kuliunganisha taifa hilo.

Jana ilikuwa ni mara ya pili kwa Kiir na Machar kukutana,mara ya kwanza ikiwa ni mwezi uliopita tarehe tisa walipotia saini makubaliano ya kusitisha mapigano,makubaliano ambayo yalisambaratika saa chache tu baada ya kutiwa saini.

Makubaliano ya awali hayakuheshimiwa

Wajumbe wa Kiir na Machar wamekuwa wakifanya misururu ya mikutano katika mahoteli ya kifahari mjini Addis Ababa tangu mwezi Januari huku pande zote mbili zikivutana na kukosa kupiga hatua zozote za tija katika kuutanzua mzozo.

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Maafisa wa IGAD wamesema mikutano hiyo ya kutafuta amani kufikia sasa imegharimu zaidi ya dola milioni 17.Katibu mtendaji wa jumuiya hiyo Mahboub Maalim awali kabla ya mkutano huo kati ya Kiir na Machar alisema kama wawili hao wanadhani watashinda kwa kufanya mashambulizi ya kijeshi basi wajue ni wajinga na kuwaelekezea lawama kuwa ndiyo wanauchochea mzozo huo.

Mapigano hayo ya Sudan Kusini yaliyozuka katikati ya mwezi Desemba mwaka jana yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimu kiasi ya watu milioni moja na laki tatu kuachwa bila makaazi.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kiasi ya watu milioninne huenda wakakabiliwa na baa la njaa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kutokana na vita hivyo kuvuruga shughuli za kilimo nchini humo.

Mwandishi:Afp/Reuters

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com