Viongozi wa RUSADA wajiuzulu | Michezo | DW | 18.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Viongozi wa RUSADA wajiuzulu

Uongozi wa shirika la Urusi la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu – RUSADA umejiuzulu huku serikali ya Urusi ikianzisha mageuzi muhimu

Hatua ya uongozi wa RUSADA infuatia ahadi ya Rais Vladmir Putin kufanya msako mkubwa dhidi ya wanariadha, wakufunzi na maafisa wanaohusika na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Hatua hiyo ndiyo ya karibuni katika mkururo wa matukio yaliyojitokeza kufuatia madai ya kashfa ya matumizi ya dawa hizo katika riadha inayogundulika kuidhinishwa na maafisa wa serikali, wakati maafisa wakiendelea kusalia na matumaini ya kuwa wanariadha wan chi hiyo watashiriki katika Michezo ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro mwaka ujao. Maafisa hao wa RUSADA wamesalimu amri baada ya onyo kutoka kwa Putin "kuna mtazamo wa pamoja kuhusiana na sheria na hasa kuhusiana na suala hili. Panahitaji kawaida kuwa na uwajibikaji wa kibinafsi. Kocha, mwandalizi wa mashindano, mwanariadha, yeyote anayestahili kulaumiwa sharti aadhibiwe. Wale wasiohusishwa na uovu huo hawapaswi kuadhibiwa. Haingii akilini, na sio haki na sio vyema. Hii ndio misingi tutakayopigania".

Russland Jahrespressekonferenz Präsident Wladimir Putin

Rais wa Urusi Vladmir Putin ametoa onyo kali

Shirika la kimataifa la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu – WADA lilichapisha ripoti ya tume huru iliyosema kuwa RUSADA ilikiuka viwango vya kimataifa vya vipimo na kuwaruhusu kushiriki mashindanoni wanariadha waliopigwa marufuku baada ya kugundulika kutumia dawa hizo. Putin ameahidi mabadiliko makubwa kuhusu hilo "Nataka kusema hili tena, Urusi lazima na itakuwa tayari kushirikiana katika kupambana na matumzii ya dawa za kuongeza misuli nguvu. Nitaamuru kutoka kwa maafisa wote, taasisi zote katika kila ngazi kushirikiana wazi na mifumo ya kimataifa, na kutoficha chochote. Tuna nia ya kutimiza hilo na tutaufuata mkondo huu".

Shirika la kimataifa la riadha – IAAF liliisimamisha kwa muda Urusi kushiriki katika michezo yote ya riadha, na RUSADA ikapigwa marufuku pamoja na maabara ya Moscow ya kufanya vipimo vya dawa za kuongeza misuli nguvu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com