Viongozi wa nchi 6 zenye nguvu duniani wazungumzia mpango wa nyuklia wa Iran | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa nchi 6 zenye nguvu duniani wazungumzia mpango wa nyuklia wa Iran

Viongozi hao wamekutana mjini Brussels kujadili hatua ya Iran kukataa mpango wa urutubishwaji wa madini yake ya uranium.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, Shoto, akiwa na Mkuu wa IAEA, Mohamed ElBaradei, mjini Tehran.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, Shoto, akiwa na Mkuu wa IAEA, Mohamed ElBaradei, mjini Tehran.

Viongozi wa mataifa sita yenye nguvu duniani, wamekutana mjini Brussels leo, kujadiliana kuhusu hatua ya Iran kuukataa mpango wa urutubishaji wa madini yake ya uranium, wakati mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki-IAEA, Mohamed ElBaradei akisema kuwa Iran haijatoa jibu la mwisho juu ya mpango huo wa kipekee.

Nchi zinazoijadili Iran

Wawakilishi wa nchi tano wenye uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani pamoja na Ujerumani, wamekutana kwa siri katika juhudi za kuishawishi Iran kuachana na mpango wake wa nyuklia. Hata hivyo, maafisa wamegoma kusema kama mataifa hayo sita watajibu hatua ya Iran, huku msemaji wa Mkuu wa sera za nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana akisema kuwa mkutano huo ni kwa ajili ya kupitia upya maendeleo ya hivi karibuni juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Mataifa ya Magharibi yamekuwa yakiishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za nyuklia, huku nchi hiyo ikikanusha tuhuma hizo ikisema kuwa nishati hiyo ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kijamii. Katika hatua ya kuhakikisha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni salama, mataifa hayo yalitoa pendekezo kwa Iran kusafirisha nje ya nchi hiyo asilimia 70 ya madini yake ya uranium ili yakarutubishwe huko. Lakini siku ya Jumatano Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Manouchehr Mottaki alisema kuwa Iran haitalikubali pendekezo hilo lililotolewa na IAEA.

Kauli ya El-Baradei

Wakati huo huo, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki, Mohamed ElBaradei amesema anaamini kuwa Iran haijakataa kabisa mpango huo wa kurutubisha madini yake ya uranium. Akizungumza leo na waandishi habari mjini Berlin, Bwana ElBaradei amesema hajapokea jibu lolote la mwisho la kimaandishi kutoka kwa Iran, lakini amesema ana matumaini kuwa atapokea jibu hilo hivi karibuni. Ameongeza kuwa suala hilo liko mikononi mwa mahakama ya Iran na kuongeza kuwa anatumai kuwa nchi hiyo haitakaa pendekezo hilo la kipekee. Bwana ElBaradei amesema jibu litakalotolewa na Iran litafungua nafasi kwa nchi hiyo na Marekani kufanya mazungumzo ya kina. Iran kwa upande wake imekuwa ikiilaumu Marekani ndiyo sababu kuu ya kukwama kwa harakati za kuyaondolea wasi wasi mataifa ya Magharibi kuhusiana na mpango wake wa nyuklia. ElBaradei ambaye anaondoka madarakani mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba baada ya kuliongoza shirika hilo kwa miaka 12, ameongeza wasi wasi juu ya Iran kuwekewa vikwazo vipya kutokana na mpango wake huo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 20.11.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Kc28
 • Tarehe 20.11.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Kc28
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com