1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia:Wakuu wa majimbo wataka kumalizwa mgogoro wa uongozi

Sudi Mnette
17 Septemba 2021

Viongozi wa majimbo Somalia wamewatolea wito rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed na waziri mkuu Mohamed Hussein Roble kumaliza uhasama baina yao ambao umezusha wasiwasi kiusalama wa taifa hilo la Pembe ya Afrika

https://p.dw.com/p/40Raf
Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed | Farmajo
Picha: Str/AFP

Mzozo huo ulionekana wazi kuongezeka jana Alhamis, baada ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed, anaejulikana sana kama Farmajo, kuyasitisha madaraka ya utendaji ya Mohamed Hussein Roble. Viongozi hao wa juu kabisa nchini humo wamekuwa wakipingana katika suala la teuzi za nafasi za maafisa wa ngazi ya juu wa usalama wa taifa. Mzozo huo unaojitokeza kwenye kipindi hiki ambacho Somalia inapambana kufanikisha uchaguzi uliochelewesha mara kadhaa, huku kukiwepo pia makabiliano ya makundi ya wenye itikadi kali za Kiislamu.

Viongozi wa majimbo wamesema kujibishana kwa matamko hakutasaidia taifa

Somalia Angriff auf African Union Soldaten
Athari za uasi nchini SomaliaPicha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Viongozi wa majimbo wa Somalia wamejitokeza na kutoa wito wa viongozi hao kuacha mara moja kurushiana maneno na badala yake, kutatua mzozo huo kwa kupitia njia ya upatanishi pamoja na kuheshimu katiba ya mpito ya taifa hilo.

Katika taarifa yao ya pamoja viongozi wa mamlaka za Jubaland, Southwest, Galmudug, Hirshabele na Puntland wameonesha kusikitishwa sana na mgogoro unaondelea katika serikali ya shirikisho ya Somalia, na kuongeza kwamba hauna manufaa kwa umma, jambo ambalo wamelitaja linazidisha wasiwasi wa kiusalama na kuteteresha hali ya kisiasa.

Somalia inahitaji uchaguzi wa haraka kumaliza mkwamo wa kisiasa

Vilevile taarifa hiyo ya viongozi hao imeitaka bodi inayoratibu mchakato wa uchaguzi wa nchi hiyo kuzidisha kasi yake. Muhula wa miaka minne madarakani kwa Farajo ulifikia ukomo wake Februari, lakini ukarefushwa na bunge la Somalia mwezi Aprili, jambo ambalo pia lilizusha mapigano makali ya kufyatuliana risasi mjini Mogadishu, baada ya wapinzani kulinganisha hatua hiyo na  kitendo cha kujinyakulia  madaraka.

Waziri mkuu Roble amejibu hatua hiyo akisema hatotii agizo hilo la rais na kumshutumu kwa kupindisha masharti ya katiba aliyotaja kuhalalisha kuingilia kwake mamlaka ya ofisi ya waziri mkuu. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu, imesema kuwa kiongozi huyo anamkumbusha raisi kuheshimu masharti ya katiba ya mgawanyo wa mamlaka kwa  taasisi za dola.

Waziri Mkuu Roble alifanya jitihada ya kuandaa ratiba mpya ya uchaguzi, ingawa mchakato wake ulishindwa kufanikishwa, na awamu nyingine pia haitafanyika hadi Oktoba Mosi, wakati uchaguzi wa bunge dogo ukitarajiwa kufanywa Novemba 25. Kimsingi uchaguzi wa Somalia unafanywa kwa namna tata ambapo wawakilishi wa majimbo pamoja na wa koo  wanawachagua wabunge wa taifa ambao wanakuwa na dhamana ya kumchagua rais wa taifa hilo.

Chanzo: AFP