Viongozi wa kimataifa wakusanyika mjini Berlin | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 09.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Viongozi wa kimataifa wakusanyika mjini Berlin

Ni katika kuadhimisha miaka 20 tangu kuanguka ukuta wa Berlin

Kutoka kushoto, Rais wa zamani wa Urusi Mikhail Gorbachev, Rais wa zamani wa Marekani George H.W Bush na Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl, wakishikana mikono kuadhimisha miaka 20 ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin.

Kutoka kushoto, Rais wa zamani wa Urusi Mikhail Gorbachev, Rais wa zamani wa Marekani George H.W Bush na Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl, wakishikana mikono kuadhimisha miaka 20 ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin.

Viongozi wa kimataifa wamekusanyika mjini Berlin leo, ikiwa ni miaka 20 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin ambao ulimaliza mtengano uliokuwepo wa Ujerumani mbili, Mashariki na Magharibi.

Novemba 9 mwaka 1989, vikwazo vya usafiri kwa raia wa Ujerumani Mashariki viliondolewa bila kutegemewa, na kusababisha maelfu ya wakaazi wa Berlin kukimbilia katika eneo la kizuizi lililoogopwa mno, ambapo waliruhusiwa kuvuka katika usiku huo uliokuwa wa shamrashamra.

Mwezi uliofuatia, eneo la Mashariki mwa Ulaya lililokuwa likidhibitiwa na Urusi ya zamani likaporomoka.

Viongozi wa mataifa makubwa manne yaliyoshiriki katika vita vya pili vya dunia, Uingereza, Ufaransa, Urusi na Marekani, wanatarajiwa kushiriki katika sherehe hizi wakiongozwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Merkel anatarajiwa kuanza siku hii kwa misa ya kumbukumbu katika kanisa la Gethsemane, ambalo lilikuwa ni kituo cha harakati za upinzani dhidi ya utawala wa kikomunisti wa Ujerumani Mashariki (GDR) katika Berlin Mashariki ya zamani.

Baadaye atashiriki katika wasaa wa kutulia na kutafakari katika Kanisa dogo la Maridhiano, lililojengwa katika eneo linaloitwa Ukanda wa Kifo, eneo lililokua marufuku baina ya pande mbili za Berlin.

Merkel, aliyekulia Ujerumani Mashariki, atazifuatilia nyayo zake katika eneo la zamani la ukaguzi kwenye daraja la Bornholmer, ambapo alikuwa ni mmoja wa kundi la watu wenye furaha waliovuka kuingia Berlin ya Magharibi mwaka 1989.

Kansela ataungana na watu mashuhuri wa mwaka huo ikiwa ni pamoja na Rais wa zamani wa Urusi Mikhail Gorbachev, kiongozi wa zamani wa upinzani nchini Poland aliyekua baadaye rais wa nchi hiyo Lech Walesa, pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu.

Tukio hili la leo litamalizika katika geti maarufu la Brandeburg, ambalo kwa miaka 28, limekuwa nje ya mipaka katikati ya majiji yaliyogawanyika.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown, Dimtry Medvedev wa Urusi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, wataungana na Merkel katika sherehe za matembezi kuelekea katika geti hilo.

Wageni wengine ni Rais wa halmashauri kuu ya Ulaya Manuel Barroso, na Rais wa bunge la ulaya Jerzy Buzek.

Kwa miaka kadhaa iliyopita, eneo la kati la Berlin limegawanywa kwa ukuta mdogo wa urefu wa mita 2.5, matofali yaliopangwa na wasanii na watoto wa shule kutoka Ujerumani na sehemu nyingine duniani.

Bw Walesa atauangusha ukuta huo , kuashiria ukubwa wa tukio, ambalo lilianza mapema mwaka 1989 nchini Poland na kusababisha kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, na kumaliza utawala wa kisovieti katika Ulaya mashariki.

Sherehe hizo pia zitapambwa na maonesho ya muziki.

Tukio hili litamalizika jioni ya leo kwa mizinga na fashifashi, kukumbuka zile sherehe za usiku mzima juu ya Ukuta wa Berlin, pale mpaka ulipofunguliwa miaka 20 iliyopita.

Mwandishi:Lazaro Matalange/DPAE/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com