1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa IGAD wakutana Addis Ababa kuijadili Sudan Kusini

Admin.WagnerD13 Machi 2014

Viongozi wa nchi za kanda ya jumuiya ya ushirikiano wa kiserikali wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika wanakutana leo,Ethiopia katika juhudi za kujaribu kutafuta amani Sudan Kusini

https://p.dw.com/p/1BOyd
Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi kutoka Jumuiya ya ushirikiano ya nchi za mashariki mwa Afrika na pembe ya Afrika IGAD wanakutana katika mji mkuu wa Ethiopia kuijadili hali ilivyo hivi sasa nchini Sudan Kusini.

Vyombo vya habari vya Sudan Kusini vimeripoti kuwa Rais Salva Kiir anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo lakini hakuna mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya Kiir na viongozi wa waasi yanayotarajiwa kufanyika hadi wiki ijayo.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi zinazoshiriki mkutano huo wa Addis Ababa walikutana hapo jana kabla ya mkutano huo wa kilele hii leo wakiwemo maafisa kutoka Djibouti,Ethiopia,Kenya,Somalia,Sudan,Sudan Kusini na Uganda.

Kujikokota kwa mazungumzo kwaangaziwa

Taarifa ya IGAD imesema maafisa hao waliijadili ripoti ya mpatanishi mkuu wa IGAD Seyoum Mesfin kuhusu hali ya kujikokota kwa mazungumzo ya kutafuta amani Sudan Kusini.

Wawakilishi wa serikali ya Sudan Kusini na waasi baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano
Wawakilishi wa serikali ya Sudan Kusini na waasi baada ya makubaliano ya kusitisha mapiganoPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Sudan Kusini imekuwa ikipambana na makundi ya waasi tangu tarehe 15 mwezi Desemba mwaka jana baada ya tofauti kuibuka kati ya Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar aliyemfuta kazi na kuzua mapigano mabaya yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha maelfu wengine bila makaazi.

Waziri mkuu wa Somalia Abdiweli Sheikh Ahmed ambaye amesema atahudhuria mkutano huo ulioandaliwa na IGAD amesema mkutano huo wa leo unanuia kushughulikia njia za kutekeleza makubaliano ya hapo awali na kutumwa kwa vikosi vya kulinda amani katika taifa hilo changa.

Mapigano bado yanaendelea licha ya makubaliano

Pande mbili zinazozozana Sudan Kusini zilitia saini makubaliano yaliyosimamiwa na IGAD ya kusitisha mapigano mnamo tarehe 23 mwezi Januari lakini mapigano makali yameendelea kuripotiwa nchini humo.

Mazungumzo ya kutafuta amani yaliyokwama mjini Addis Ababa kati ya serikali na waasi na ambayo hayajapiga hatua zozote za kuridhisha yanatarajiwa kuanza tena tarehe 20 mwezi huu.

Kambi za wakimbizi wa Sudan Kusini
Kambi za wakimbizi wa Sudan KusiniPicha: Reuters

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn wiki hii amesema mchakato huo wa kutafuta amani unakwenda mwendo wa pole pole mno lakini yako katika mkondo ulio sawa.

Kulingana na Umoja wa Mataifa,zaidi ya raia 930,000 wametoroka makaazi yao tangu mapigano hayo yalipoanza wakiwemo zaidi ya raia laki mbili waliokimbilia nchi jirani kama wakimbizi.

Mkutano huo wa IGAD unakuja siku moja tu baada ya Umoja wa Afrika kuanzisha uchunguzi maalumu kuhusu uhalifu uliofanywa Sudan Kusini yakiwemo mauaji yaliyochochewa kikabila.

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ambaye aliapishwa kuwa kiongozi wa tume hiyo ya uchunguzi yenye nchi wanachama wa tano wa umoja wa Afrika ameapa kuwa yeyote aliyehusika katika vita vya Sudan Kusini hataachiwa kuwa huru kufanya uhalifu bila ya kujali.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu