1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa IGAD wajadili Sudan Kusini

27 Desemba 2013

Viongozi wa Afrika Ijumaa(27.12.2013) wanazungumzia mzozo unaozidi kukuwa Sudan Kusini wakati Umoja wa Mataifa ukiharakisha uwekaji wa vikosi zaidi nchini humo kukomesha umwagaji damu katika taifa hilo changa kabisa.

https://p.dw.com/p/1AhO4
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn(kushoto) Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini(katikati) na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya(kulia)wakiwa mjini Juba Alhamisi(26.12.2013).
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn(kushoto) Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini(katikati) na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya(kulia)wakiwa mjini Juba Alhamisi(26.12.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya hapo jana walikutana na Rais Salva Kiir mjini Juba na kusema kwamba wamepiga hatua nzuri za maendeleo kwa kwa kile walichokitaja kuwa mazungumzo ya amani. Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Kanda IGAD wanatarajiwa kukutana mjini Nairobi leo hii kuendeleza juhudi za kukomesha mzozo wa umwagaji damu wa kikabila unaopamba moto Sudan Kusini.

Hali ya mvutano katika nchi hiyo iliojipatia hurun wake kutoka Sudan miaka miwili tu iliopita ilikuja kuripuka kuwa mzozo wa umwagaji damu hapo Disemba 15 kwa mapambano makali kati ya vikosi vilivyo tiifu kwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na vile vinavyomuunga mkono makamo wake Riek Machar aliyetimuliwa madarakani. Mapigano hayo sasa yamezagaa hadi kwenye majimbo kumi ya nchi hiyo.

Juhudi kukomesha umwagaji damu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Jumanne limekubali kuongeza takriban maradufu ukubwa wa kikosi chake cha kulinda amani kinachojulikana kama UNMISS ili kuweza kufikia wanajeshi 12,500 na polisi 1,300 baada ya mzozo huo kuonekana kushindwa kudhibitika.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini(UMINSS) wakiwa katika doria kwenye eneo lao kwenye viunga vya Juba.
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini(UMINSS) wakiwa katika doria kwenye eneo lao kwenye viunga vya Juba.Picha: Reuters

Wakati jumuiya ya kimataifa ikiwa mbioni kuizuwiya nchi hiyo kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe Umoja wa Mataifa hapo jana umetangaza kwamba vikosi vya ziada na zana muhimu za kijeshi kama vile helikopta zitakuwa zimewekwa nchini humo kufikia hapo kesho.

Hilde Johnson ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Sudan Kusini amesema wanaongeza wafanyakazi wao kwenye maeneo muhimu yanaohitaji usalama na kuimarisha kambi zao zinazohitaji kuimarishwa kijeshi.Amesema hiyo ina maana kwamba wanahamisha wanajeshi wao wa kulinda amani kutoka maeno ambayo hivi sasa hayana umuhimu na kuwapeleka kwenye kambi zao za Juba,Bor na Bentiu.

Mapambano yanaendelea

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Philip Aguer ameliambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi vyake vinapambana na vikosi vyenye kumuunga mkono Machar ndani ya mji wa Malakal ambao ni mji mkuu wa jimbo la Upper Nile.Pia amesema vikosi hivyo vinajiandaa kuushambulia mji wa Bentiu mji mkuu katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Unity.

Familia zilizopoteza makaazi zikiwa kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa huko Jabel kwenye kiunga cha mji mkuu wa Juba.
Familia zilizopoteza makaazi zikiwa kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa huko Jabel kwenye kiunga cha mji mkuu wa Juba.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa maelfu ya watu wameuwawa na zaidi ya watu 120,000 wamepotezewa makaazi kutokana na kuendelea kwa mzozo huo wa umwagaji damu ambapo nusu yake wanatafuta hifadhi kwenye kambi za Umoja wa Mataifa nchini humo. Huku kukiwa na repoti za maiti kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja na ushahidi wa watu kunyongwa na kubakwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameahidi wale waliohusika na vitendo hivyo watawajibishwa.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mwandishi:Abdul-Rahman