Viongozi wa G7 waitenga Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa G7 waitenga Urusi

Mkutano wa kilele kuhusu usalama wa nyuklia unaoyahusisha mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda duniani-G7, leo unaingia siku yake ya pili na ya mwisho mjini The Hague, Uholanzi.

Viongozi wa kundi la G7

Viongozi wa kundi la G7

Siku ya ufunguzi hapo jana, mkutano huo ulitawaliwa na mzozo unaondelea wa Crimea, huku mataifa ya Magharibi na Japan yakisitisha ushirikiano wake na Urusi katika kundi la G8.

Viongozi wa mataifa yanayoliunda kundi la mataifa 7 yaliyoendelea kiviwanda duniani-G7, ya Marekani, Japan, Ujerumani, Italia, Ufaransa, Canada na Uingereza, wametoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa kundi la G8 linaloijumuisha Urusi halitakutana, hadi Urusi itakapobadilisha sera zake kuhusu Crimea na kwamba mkutano uliopangwa kufanyika mjini Sochi mwezi Juni mwaka huu, sasa utafanyika mjini Brussels, na Urusi haitahudhuria mkutano huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov

Awali mkutano huo wa viongozi hao, ulikuwa uzingatie zaidi kuhusu masuala ya usalama wa nyuklia, lakini badala yake umetawaliwa na hatua ya Crimea kujitenga na Ukraine na kujiunga na Urusi na uwezekano wa kuiwekea vikwazo Urusi.

Katika taarifa hiyo ya pamoja, viongozi hao wamesema wako tayari kuchukua hatua ikiwemo kuweka vikwazo vya kiuchumi, iwapo Urusi itaendelea kuukuza mzozo wa Crimea. Taarifa hiyo imefafanua kwamba kulingana na hali hiyo, hawatohudhuria mkutano wa Sochi na watasitisha ushiriki wao katika kundi la G8 ambalo limedumu kwa miongo miwili.

G7 yaiunga mkono Ukraine

Viongozi hao wamesema wanasimama imara kuwaunga mkono watu wa Ukraine, ambao wanajaribu kurejesha hali ya umoja, demokrasia, utulivu wa kisiasa na mafanikio ya kiuchumi kwa nchi yao. Aidha, taarifa hiyo imeipinga vikali kura ya maoni ya Crimea iliyosababisha rasi hiyo kujiunga na Urusi, ikisema kuwa imekiuka sheria za kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kutolewa kwa taarifa ya pamoja ya viongozi wa G7, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema G8 siyo klabu rasmi na kwamba hakuna kadi za kujiunga na uwanachama na hakuna mtu anayeweza kumuondoa mtu mwingine kwenye kundi hilo.

Rais wa China, Xi Jinping na Rais Barack Obama

Rais wa China, Xi Jinping na Rais Barack Obama

Ama kwa upande mwingine, kabla ya kukutana na viongozi wa G7, Rais Barack Obama wa Marekani alifanya mazungumzo na Rais Xi Jinping wa China. Nchi hiyo ambayo ni mshirika wa Urusi, haikupiga kura kuhusu azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa likidai kuwa kura ya maoni ya Crimea kujiunga na Urusi haikuwa halali.

Wakati huo huo msemaji wa Rais Vladimir Putin, amesema leo kuwa Urusi bado inataka kuendelea na uhusiano na mataifa ya kundi la G8 katika maeneo yote. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Urusi kutengwa na G8 tangu ilipojiunga na kundi hilo mwaka 1998.

Mapema jana Ukraine iliwaamuru wanajeshi wake kuondoka Crimea, baada ya rasi hiyo kujitenga na Ukraine na kujiunga na Urusi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,AFPE,APE,RTRE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com