1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G20 wakutana Antalya, Uturuki

15 Novemba 2015

Kushirikiana kukabiliana na ugaidi, kuratibu uhamiaji na kuusuluhisha mzozo wa Syria ni miongoni mwa maazimio yanayotarajiwa kutoka katika mkutano wa wakuu wa nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani unaofanyika Uturuki.

https://p.dw.com/p/1H69G
G-20-Gipfel in Antalya - Gruppenbild
Viongozi wa mataifa ya G20 katika picha ya pamojaPicha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Viongozi wa nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani (G20)wamekubaliana kuimarisha ulinzi mipakani na ukaguzi katika safari za ndege. Hayo ni baadhi ya maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa nchi hizo unaofanyika katika mji wa Antalya nchini Uturuki, ambao unaghubikwa na wingu la mashambulizi ya kigaidi yaliyouwa watu 129 mjini Paris Ijumaa wiki hii.

Mkutano huo unawashirikisha viongozi wa nchi zenye utajiri na ushawishi mkubwa duniani, akiwemo rais w Marekani Barack Obama, rais wa Urusi Vladimir Putin, rais wa China Xi Jinping na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon miongoni mwa wengine wengi. Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameahirisha kushiriki katika mkutano huo, wakati nchi yake ikiomboleza watu wake waliouawa katika mashambulizi hayo ya umwagaji damu mkubwa.

Mshikamano na Ufaransa

Akizungumza mjini Antalya, rais Barack Obama amesisitiza mshikamano na Ufaransa, katika kuwawinda na kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika katika mashambulizi mjini Paris. Mashambulizi hayo na yale yaliyofanyika mjini Ankara, Uturuki mwezi uliopita, hayakuzilenga nchi hizo tu, bali ''ulimwengu mzima wa wastaarabu'' na kuahidi ''kuzidisha juhudi maradufu'' katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

G-20-Gipfel in Antalya Obama und Erdogan
Rais Barack Obama wa Marekani, na mwenyeji wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture alliance/Turkish Presidency/Y. Bulbul/Anadolu Agency

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametaka hatua zote zitakazochukuliwa kujibu mashambulizi hayo katika mji mkuu wa Ufaransa, yasikiuke misingi ya sheria, akionya kuwa ikiwa misingi hiyo itapuuzwa, itakuwa kama ''kumwaga mafuta kwenye moto katika juhudi za kuuzima''.

Katibu Mkuu Ban hali kadhalika amewaasa viongozi wa G20 kuendeleza msukumo uliopo hivi sasa katika kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Syria, akisema hii ni ''fursa adimu'' ambayo inapaswa kutumiwa ipasavyo.

Viongozi wakuna vichwa kuhusu uhamiaji

Suala jingine lililopewa kipaumbele katika mkutano huo ni lile la uhamiaji, ambalo kwa wakati huu linawakosesha usingizi viongozi wa Ulaya. Nchi za G20 zimekubaliana kuwa uhamiaji kwa sasa ni tatizo la dunia, ambalo linahitaji kuratibiwa kwenye ngazi ya kimataifa.

Paris nach den Anschlägen
Mashambulizi ya kigaidi yaliyouwa watu 129 mjini Paris yameughubika mkutano huo wa G20Picha: DW/L. Scholtyssek

Viongozi wametoa wioto kwa kila nchi kutoa mchango wake katika kuishughulikia changamoto hiyo. Inatarajiwa kwamba wahamiaji wapatao milioni moja kutoka Ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika wataingia barani Ulaya mwaka huu pekee.

Ulaya na Uturuki ndizo zinazozongwa pakubwa na changamoto za uhamiaji, na zimekuwa zikishinikiza utambuliwe kama tatizo linalohitaji kuchangiwa kifedha na dunia nzima katika kukabiliana nalo, shinikizo ambalo limepingwa na China, India na Urusi.

Syria pia yaangaziwa

Mzozo wa Syria pia umekuwa agenda nyingine muhimu kwenye mkutano huo. Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk ambaye pia anahudhuria, amezitaka Urusi na Marekani kushirikiana katika operesheni zao dhidi ya Dola la Kiislamu nchini Syria, ili kufanikiwa kulitokomeza kundi hilo.

''Hatua za Urusi kuwashambulia wapinzani wa rais Bashar al-Assad wa Syria, hazisaidii chochote mbali na kuongeza idadi ya watu wanaoikimbia Syria''. Amesema Tusk.

Kwa mara ya kwanza tangu Urusi ilipojiingiza kijeshi katika mzozo wa Syria, rais wake Vladimir Putin na mwenzake wa Marekani Barack Obama, wamesalimiana na kuzungumza kwa sekunde sita. Hiyo ni hali mpya katika uhusiano baina ya mataifa hayo makubwa, ambao mnamo wa miezi ya hivi karibuni yamekuwa yamezorota mno.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/ape/afpe

Mhariri: Sudi Mnette