1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU na nchi za Kiarabu wataka suluhisho la pamoja

John Juma Mhariri: Mohammed Khelef
25 Februari 2019

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu wamemaliza mkutano wao huku wakiahidi kuimarisha ushirikiano kati yao na kutafuta masuluhisho ya pamoja ya matatizo ya kikanda.

https://p.dw.com/p/3E4HI
Ägypten Gipfel EU und Arabische Liga in Sharm El Sheikh PK
Picha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Mkutano wa kilele wa siku mbili ambao ni wa kwanza kuwahi kufanyika kati ya viongozi wa Umoja wa Ulaya pamoja na wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu umemalizika leo nchini Misri huku viongozi hao wakikubaliana kuimarisha ushirikiano wao.

Kwenye taarifa yao ya pamoja kuhusu yale waliyokubaliana, viongozi hao wamesema wamejitolea kuanzisha enzi mpya ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Pande hizo mbili, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, zimekubaliana kuandaa mikutano ya kilele ya mara kwa mara, huku mkutano ujao ukiwa umepangwa kufanyika Brussels mwaka 2022.

Mkutano huo wa ngazi ya juu wa wakuu wa nchi na serikali na ambao umefanyika katika eneo la Kitalii la Misri Sharm el-Sheikh, umejiri wakati baadhi ya nchi za Kiarabu zikikumbwa na migogoro ya kiusalama na kiuchumi huku Ulaya ikikabiliwa na ongezeko la chuki dhidi ya wahamiaji.

Mchakato wa kuwarudisha wahamiaji wa Syria makwao

Kansela wa Ujerumani akiwa ameketi na mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz wakati wa mkutano wa kwanza wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu Sharm el Shekh Misri.
Kansela wa Ujerumani akiwa ameketi na mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz wakati wa mkutano wa kwanza wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu Sharm el Shekh Misri.Picha: Getty Images/Handout/Bundesregierung/G. Bergmann

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewataka viongozi wa nchi za Kiarabu kuunga mkono mchakato wa mabadiliko ya kisiasa nchini Syria ili raia milioni sita wa nchi hiyo ambao walikimbia nchi yao, waweze kurudi makwao.

Akizungumza kwenye mkutano huo, bibi Merkel amesema viongozi wa Umoja wa Ulaya pamoja na wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu wanapaswa kubuni katiba mpya na waanze mdahalo wa kujumuisha pande zote kuhusu jinsi mustakabali wa Syria kisiasa utakavyokuwa. Kuhusu uhamiaji ambayo ilikuwa miongoni mwa ajenda kuu Merkel amesema:

"Hizi ni nchi ambazo ni majirani, na hatima ya Umoja wa Ulaya kwa kiwango fulani hutegemea hatima ya nchi za jumuiya ya Kiarabu. Tumeshuhudia hilo kwenye suala la uhamiaji. Kwa hivyo kazi yetu ni kuimarisa ushirikiano na kila mmoja, japo kuna baadhi ya masuala ambayo kuna mitazamo tofauti"

Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Ulaya Donald Tusk (Kushoto) na rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi wakihutubia mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nchini Misri.
Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Ulaya Donald Tusk (Kushoto) na rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi wakihutubia mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nchini Misri.Picha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Katika hotuba yake kuufunga mkutano huo, Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi ambaye alikuwa mwenyeji ameupongeza mkutano huo, japo pia alitambua ukosefu wa makubaliano kuhusu baadhi ya masuala ambayo hakuyataja.

Tusk apendekeza kurefushwa muda wa Brexit

Mada nyingine iliyoibuka pembezoni mwa mkutano huo ni kuhusu suala la Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya Brexit.

Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema kuchelewesha muda wa Brexit ambayo ni Machi 29, ndiyo hatua bora kwa sababu hakuna wabunge wa kutosha katika bunge la Uingereza kuidhinisha mpango wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya.

Tusk amesema kulingana na hali ilioko sasa, anaamini kuwa kurefusha muda huo ndiyo suluhisho ili kuepuka mvurugano, lakini waziri mkuu wa Uingereza Theresa May angali anaamini kuwa atafanikiwa kuepuka urefushaji wa tarehe.

Vyanzo: DPAE, AFPE