1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU na Nchi za kiarabu kuimarisha ushirikiano

John Juma Mhariri: Mohammed Khelef
25 Februari 2019

Viongozi wa Umoja wa Ulaya pamoja na wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamejadiliana kuhusu namna ya kuimarisha vita dhidi ya ugaidi, kukabiliana na uhamiaji usiokubalika na kuimarisha ushirikiano wao kiuchumi.

https://p.dw.com/p/3E2VW
Ägypten Sharm el Sheikh Gipfel von EU und Arabische Liga
Picha: Getty Images/D. Kitwood

Viongozi kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wameahidi kuimarisha ushirikiano katika biashara na vita dhidi ya ugaidi na pia kukabiliana na uhamiaji usiokubalika. Viongozi hao wameyasema hayo katika mkutano wa kilele ambao ni wa kwanza kuwahi kufanyika kati yao.

Rais Abdel-Fatah el-Sissi wa Misri aliufungua mkutano huo wa kilele katika eneo la kitalii la Sharm el Shekh nchini Misri huku ulinzi ukiwa umeimarishwa maradufu. Kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili, Rais Sissi alisifia kile alichokitaja kuwa ushirikiano wa kihistoria kati ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, huku akitolea wito wa kuwepo hatua kali za kupambana na ugaidi:

"Ninashangazwa sana, ndugu zangu na marafiki, je muda haujawadia wa kuafikia mpango wa pamoja wa kupambana na ugaidi? Mpango unapaswa kujumuisha hatua kali za kiusalama dhidi ya makundi ya kigaidi na vitendo vya kigaidi na uwezo wa kukabili mawazo ya kigaidi na pia uungwaji mkono wa vita hivyo." Amesema Rais el-Sissi

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi
Rais wa Misri Abdel Fattah el-SissiPicha: Getty Images/AFP/M. El-Shahed

Kukomesha uhamiaji usiokubalika

Mada kuhusu uhamiaji pia ilijadiliwa, huku Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, akisema ni lazima wadau wote kuhusu uhamiaji washirikiane kuvunja mbinu na mipango ya wasafirishaji haramu wa wanadamu. Pia alitaka pawepo ushirikiano thabiti kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Kiarabu, akisema kuna sababu za msingi na hilo si hiari bali lazima. Tusk ameendelea kusema kuwa "Ni azima tufanye kazi kwa ushirikiano na nchi ambazo wahamiaji hutokea, wanazopitia na nchi wanazoelekea ili kuvunja mpango wa walanguzi na wasafirishaji haramu wa binaadamu, wanaowarai watu kujiingiza kwenye safari hatari na kuendeleza utumwa mamboleo, kama njia ya kukabili uhamiaji usiokubalika."

Mkutano huo wa kilele unajiri wakati nchi za Kiarabu zinakabiliwa na migogoro ya kisiasa na kiuchumi, huku nchi za Ulaya pia zikikabiliwa na ongezeko la chuki dhidi ya wahamiaji.

Katika mkutano huo, Mfalme Salman wa Saudi Arabia amesisitiza umuhimu wa kupatikana suluhisho la kisiasa nchini Yemen, huku akiwataja waasi wa kihouthi wanaosaidiwa na Iran kuwa ni magaidi.

Hofu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa IS

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya nchi za Kiarabu kule Sharm el Shekh nchini Misri.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya nchi za Kiarabu kule Sharm el Shekh nchini Misri.Picha: picture-alliance/dpa/O. Weiken

Katika miezi ya hivi karibuni kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, limepata pigo kubwa la kijeshi nchini Iraq na Syria kufuatia mashambulizi dhidi yake. Hata hivyo, kuna hofu kuwa wapiganaji wachache wa IS waliosalia huenda wakalipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi Ulaya na Mashariki ya Kati.

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini aliwaambia waandishi habari kwamba anatarajia mkutano huo wa kilele utafanikiwa kujikita katika kuangalia ushirikiano kati ya pande hizo mbili kuhusu mahusiano ya kiuchumi na ushirikiano kuhusu suala la Palestina na migogoro ya Syria na Yemen.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wengi mashuhuri akiwemo Kansela  Angela Merkel wa Ujerumani.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wamehoji kuwa huenda mkutano huo usizae matunda makubwa yanayotarajiwa kufuatia tofauti zilizoko kati ya pande mbili husika.

Kwenye hotuba yake, Donald Tusk alisema anatambua kuna tofauti kati ya pande hizo mbili na hivyo hawahudhurii mkutano huo kwa kujidanganya kuwa wanakubaliana katika kila jambo. Lakini ni kwa sababu wote wanakabiliwa na changamoto sawa zinazohitaji ushirikiano wao kwa pamoja.

Vyanzo: APE, DPAE