1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU kujadili ulinzi, China, Marekani

Angela Mdungu
5 Oktoba 2021

Viongozi  wa Umoja wa Ulaya, wanakutana leo kwa mara ya kwanza tangu wanajeshi wa nchi za magharibi walipoondoka Afghanistan, na tangu Ufaransa ilipopoteza mkataba wa mamilioni wa nyambizi za kivita na Australia

https://p.dw.com/p/41IFR
EU Flagge
Picha: picture-alliance/NurPhoto/N. Economou

Viongozi hao 27 wa Umoja wa Ulaya katika mkutano huo unaofanyika kwenye kasri la Brdo, karibu na mji mkuu wa Slovenia, Ljubljana watakuwa na mengi ya kujadili. Mazungumzo hayo yasiyo rasmi hayatarajiwi kuwa na matokeo thabiti bali yanalenga kuandaa msingi wa mkutano wa siku mbili utakaofanyika baadaye mwezi huu mjini Brussels.

Kwa mujibu wa kauli ya mapema leo ya Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen viongozi hao wanatarajiwa pia kuzungumzia wazo la kuanzisha hifadhi ya gesi katika umoja huo.

Pamoja na masuala ya usambazaji wa gesi na kuanguka kwa uchumi nchini Afghanistan mkutano huo unatarajiwa kutafakari upya uhusiano wa Umoja wa Ulaya  na China mada ambayo haijauzungumzia kwa pamoja kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Katika mazungumzo ya mwisho ya viongozi wa Umoja wa Ulaya walianzisha mpango mkubwa wa uwekezaji na China lakini pia walipitisha vikwazo dhidi ya maafisa wa nchi hiyo kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo la magharibi la Xinjiang.

Watajadili pia makubaliano ya AUKUS

Viongozi hao watasikia pia kutoka kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu namna umoja huo unavyoweza kujaribu  kuongeza uwezo wake katika masuala ya kimataifa baada ya Uingereza, Marekani na Australia kukubaliana kwa siri kuikabili China kwa kuunda muungano wa kijeshi bila kuishirikisha Ufaransa.

Belgien EU-Gipfel l Französischer Präsident Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: John Thys/AP/picture alliance

Muungano huo unaojulikana kama AUKUS ulisababisha Australia iachane na mkataba wake wa kupata nyambizi za kielektroniki za Ufaransa, badala yake itajipatia manowari zake kutoka Marekani badala ya Ufaransa. Hatua hiyo ya Australia imeikasirisha Ufaransa, ambayo inatafuta ufafanuzi kutoka kwa Marekani juu ya wajibu wake kwa washirika wake wa Ulaya.

Nchi kadhaa wanachama  wa Umoja wa Ulaya  zimeonesha kuiunga mkono Ufaransa. Kwa sasa Macron, ametoa wito kwa washirika wa Umoja wa Ulaya watumie makosa yaliyofanywa na umoja huo katika suala la Afghanistan pamoja na kuibuka kwa AUKUS kama nafasi ya kujisahihisha kwa kutengeneza mfumo wa kujilinda wa nchi za Ulaya na kuboresha uhusiano wake na Marekani wakati huohuo.

Katika mkutano huo wa siku mbili, viongozi hao wa Umoja wa Ulaya wataungana na wenzao kutoka nchi sita za Balkani ambazo zina matumaini ya kujiunga na Umoja huo.