Viongozi wa EU kujadili hali ya hewa, Ebola | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa EU kujadili hali ya hewa, Ebola

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo Brussels kujadili sera mpya ya nishati, ambayo inaazimia kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa inayochafua mazingira na kuongeza joto ulimwenguni.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watajadili sera mpya ya matumizi ya nishati yasiyoharibu mazingira

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watajadili sera mpya ya matumizi ya nishati yasiyoharibu mazingira

Katika mkutano huo, viongozi wa mataifa 28 wanachama wa umoja huo wanataka kutoa mfano kuelekea makubaliano ya kimataifa yanayyotarajiwa kutiwa saini mjini Paris mwaka ujao, baina ya nchi zilizoendelea kiviwanda ya Ulaya, Amerika Kaskazini na Asia kwa upande mmoja, na nchi zinazoendelea kutoka maeneo mengine ya dunia kwa upande mwingine.

Makubaliano hayo ya Paris yatakuwa na lengo la kuboresha ushirikiano ambao umesuasua kwa miongo miwili iliyopita, ili kupunguza kiwango cha utoaji wa hewa ya ukaa ambayo inalaumiwa kwa ongezeko la haraka la joto ulimwenguni.

Washiriki wengi katika mkutano huo wanaunga mkono nia ya kupunguza hewa ukaa itokayo viwandani, majumbani na kwenye magari barani Ulaya kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2030, kulinganisha ni kiwango cha mwaka 1990, mwaka ambao kiwango cha hewa hiyo kilianza kukithiri duniani.

Njia ndefu kuelekea muafaka

Utoaji wa kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa umelaumiwa kupandisha kiwango cha joto duniani

Utoaji wa kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa umelaumiwa kupandisha kiwango cha joto duniani

Hata hivyo wanadiplomasia wanasema tofauti za kimaoni kuhusu kuzisaidia nchi maskini za mashariki mwa Ulaya, au kupendelea nishati ya atomiki kuliko ile endelevu itokanayo na jua na upepo, inaweza kuukwamisha mkutano huo, na kuurefusha hadi usiku, au hata kesho Ijumaa.

Kwa wakati huu, kiwango cha utoaji wa hewa ya Ukaa katika nchi za Umoja wa Ulaya kimepungua kwa asilimia 20 kikilinganishwa na cha mwaka 1990.

Lakini baada ya miaka sita ya mkwamo wa uchumi, nchi nyingi, hususan zile zinazotegemea makaa ya mawe kama chanzo chao kikuu cha nishati kama Poland, zinahofia kuwa kupunguza viwango hivyo vitaathiri sana bajeti zao, hali ambayo inaweza kuzigharimu kisiasa.

Uingereza kukataa shinikizo

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron anatarajiwa kupinga shinikizo la kuheshimu viwango vya Ulaya

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron anatarajiwa kupinga shinikizo la kuheshimu viwango vya Ulaya

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ni miongoni mwa viongozi ambao hawataki shinikizo kubwa kuzilazimisha nchi kuheshimu viwango vinavyolengwa. Anaazimia kubakia na nishati inayozalishwa na vinu vya nuklia, kwa hofu kuwa kukubaliana na kila hatua ya Umoja wa Ulaya kwaweza kuwaimarisha wanasiasa wanaoupinga umoja huo nchini Uingereza.

Maafisa wanasema kile ambacho viongozi wa Ulaya wanaweza kukifikia, ni muafaka juu ya mpango wa dunia ambao unaweza kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa bila kuathiri uchumi kwa kiwango kikubwa.

Mbali na suala hilo la sera ya pamoja kuhusu utunzaji wa mazingira, viongozi hao wa Ulaya wanatarajiwa kuidhinisha msaada zaidi kwa nchi za kiafrika zinazokabiliwa na janga la maradhi ya Ebola.

Mgogoro wa Ukraine ni suala jingine muhimu ambalo litakuwa kwenye meza ya mazungumzo ya viongozi hao, hasa kuiwekea mbinyo Urusi ili itoe mchango bora zaidi katika kumaliza uhasama kati ya serikali ya Ukraine na waasi wa mashariki wanaotaka kujitenga, na ambao wanaegemea upande wa Urusi.

Hasli kadhalika nchi wanachama wa kanda inayotumia sarafu ya Euro watazungumza juu ya matatizo ya kiuchumi yanayozikabili, lakini kutokana na maoni yanayokinzana baina ya Ufaransa na Ujerumani, nchi mbili zinazoongoza kiuchumi katika kanda hiyo, hakuna uamuzi wowote unaotarajiwa kufikiwa kuhusu hatua za kubana matumizi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com