1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Viongozi wa dunia waisihi Israel kuacha operesheni ya Rafah

Bruce Amani
15 Februari 2024

Jumuiya ya kimataifa imeongeza shinikizo la kuupinga mpango wa Israel wa kufanya kile imekitaja "operesheni kubwa" kwenye mji wa Rafah ulio kusini mwa Gaza eneo ambalo zaidi ya Wapalestina milioni 1.3 wamekwama.

https://p.dw.com/p/4cQx9
Israel | Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu Netanyahu ameaviagiza vikosi vyake kujiandaa kuivamia Rafah.Picha: Ohad Zwigenberg/AFP/Getty Images

Jumuiya ya kimataifa imeongeza shinikizo la kuupinga mpango wa Israel wa kufanya kile imekitaja "operesheni kubwa" kwenye mji wa Rafah ulio kusini mwa Gaza eneo ambalo zaidi ya Wapalestina milioni 1.3 wamekwama bila ya kuwa na mahali pengine pa kwenda.

Australia, Canada na New Zealand ndiyo mataifa ya hivi karibuni kabisa kuonya dhidi ya mpango wa operesheni ya ardhini inayoandaliwa naIsrael kwenye mji wa Rafah, yakionya kwamba operesheni kama hiyo itasababisha janga kubwa kwa raia.

Akizungumza jana usiku kabla ya kuelekea Israel, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock alisema operesheni kama hiyo italeta balaa kubwa na kuifanya hali ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Gaza kupindukia kiwango kisichomithilika.

Soma pia: Israel yatahadharishwa dhidi ya kuanza kushambulia Rafah

Waziri Mkuu wa Israel Israel Benjamin Netanyahu amesema watapambana hadi wapate ushindi na hilo litajumuisha hatua kali ya kijeshi huko Rafah baada ya kuwaruhusu raia kuondoka.

Mjini Cairo, wapatanishi kutoka Marekani, Qatar na Misri wanaendelea kutafuta makubaliano yatakayowezesha kusitishwa mapigano na kuruhusu kuwachiwa kwa karibu mateka 130 wanaoshikiliwa Gaza kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel.