Viongozi wa dunia waanza kuwasili Copenhagen | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 16.12.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Viongozi wa dunia waanza kuwasili Copenhagen

Viongozi wa dunia wameanza kukusanyika mjini Copenhagen, huku polisi wakiwakamata waandamanaji 100 waliotishia kuuvuruga mkutano huo wa hali ya hewa.

default

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ahutubia waandishi wa habari, Copenhagen.

Viongozi wa dunia wameanza kukusanyika mjini Copenhagen, katika mkutano wa hali ya hewa, siku moja tu baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuwashinikiza watumie fursa hii ya kihistoria kupata mkataba wa kukabiliana na athari za ongezeko la ujoto duniani. Wakati huo huo polisi wamewakamata zaidi ya waandamanaji 100 waliokuwa wakielekea katika ukumbi huo wa mkutano huo, huku wapatanishi zaidi ya 200 wakijaribu kupata ufumbuzi wa kukwama kwa juhudi za kupata mkataba wa kimataifa.

Klimagipfel Copenhagen Proteste

Waandamanaji waandamana, Copenhagen

Wajumbe mjini Copenhagen wana siku tatu tu, ya kuafikiana kuhusiana na mkataba wa kimataifa wa hali ya hewa, lakini mzozo baina ya nchi mbili muhimu katika mazungumzo hayo, unatishia kuwa chanzo cha kufeli kwa mkutano huo Copenhagen.

China na Marekani, nchi mbili ambazo zinatoa gesi nyingi ya kuharibu mazingira, duniani, zimepuuzilia mbali mwito wa Bara la ulaya kuhusiana na viwango watakavyopunguza vya gesi inayoharibu mazingira- swala ambalo limekuwa tete katika mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa.

Na huku Copenhagen ikianza kuwapokea viongozi zaidi 120, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliwaambia wanakabiliwa na fursa ya kihistoria, mjini Copenhagen- kuondoka na mkataba ambao utaweka maanani maslahi ya kila upande.

Mkutano huo wa Umoja wa mataifa, unalenga kupata lengo la muda mrefu la kupunguza gesi zinazoharibu mazingira, upunguzaji wa ongezeko la ujoto duniani na mpango wa kutoa fedha kwa mataifa maskini ambayo yanakabiliwa na janga la njaa, mafuriko, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwanamfalme Charles kutoka Uingereza, aliwaambia viongozi, muda unakwenda mbio, ilhali mazungumzo yanaonekana kukwama, na hili litasababisha viongozi wakuu wanaoanza kufika Copenhagen kuwa na wakati mgumu wa kupata maafikiano yeyote.

Klimagipfel Copenhagen Proteste

Mivutano ya utendaji imegubika mkutano wa hali ya hewa, Copenhagen.

'' Kama ilivyo kwa binadamu kwamba wana uwezo wa kuiweka dunia ukingoni, pia tuna uwezo wa kuirejesha katika hali nzuri. Mwewekwa mwanadamu mabibi na mabwana katika nafasi ya uwajibikaji katika wakati huu muhimu. Macho ya ulimwengu yako kwenu na sio jambo la mzaha kusema, kwa kutia kwenu saini mnaweza kuilekeza hali yetu ya baadaye.'' Alisema Charles.

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown pamoja na Rais Robert Mugabe ni baadhi ya viongozi watakaohutubia wajumbe baadaye leo.

Masuala haya ya msingi yanajadiliwa kwa makundi mbali mbali ikiwemo mawaziri wa mazingira, katika matumaini ya kupata muafaka ifikapo siku ya Ijumaa, kabla ya makubaliano kuwasilishwa kwa viongozi kutoka duniani kote. Kuwasili kwa viongozi wakuu, kunatarajiwa kupiga jeki majadiliano hayo ya siku 12 ambayo yamegubikwa na mivutano ya kiutendaji na kunyosheana vidole.

Wakati huo huo, Polisi mjini Copenhagen wamewakamata waandamanaji kiasi cha 100, waliokuwa wanaelekea katika ukumbi wa mkutano huo, kupaaza sauti zao, kuwa mkutano Copenhagen haupaswi kufeli.

Mwandishi: Munira Muhammad/ DPAE

Mhariri: Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com