Viongozi wa dini Afrika ya kati walia na UN | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa dini Afrika ya kati walia na UN

Viongozi wa dini za Kikristu na Kiislamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameuomba Umoja wa Mataifa kupeleka mara moja vikosi vya kulinda amani ili kuzuwia kusambaa kwa ghasia zinazowapambaisha Wakristu na Waislamu.

Wanajeshi wa kulinda amani wakifanya doria mjini Bangui.

Wanajeshi wa kulinda amani wakifanya doria mjini Bangui.

Katika makala ya maoni iliyochapishwa katika gazeti la Le Monde la nchini Ufaransa, Askofu mkuu wa Bangui, Dieudonne Nzapalainga, na imamu Omar Kobine Layama, walisema vikosi vya Ufaransa na Umoja wa Afrika vinahitaji msaada ili kukomesha ghasia.

"Umoja wa Mataifa unapaswa kutuma kikosi hicho mara moja," walisema katika makala yao ya pamoja. Ufaransa ilituma wanajeshi 1,600 katika koloni lake hilo la zamani kusaidiana na vikosi vya Umoja wa Afrika karibu 4,000. Lakini wanajeshi hao wamekuwa wakihangaika kurejesha utulivu katika taifa hilo lililopitia miongo kadhaa ya utawala mbovu, mapinduzi na udikiteta.

Waandamanaji wakiwa na mabango ya kupinga vikosi vya Chad na Seleka.

Waandamanaji wakiwa na mabango ya kupinga vikosi vya Chad na Seleka.

Jeshi la Chad lapingwa
Na katika hatua inayozidi kutatiza juhudi za amani, kombania ya wanajeshi wa Chad imelaumiwa kwa kuungana na waasi wa zamani wa muungano wa Seleka, ambao wengi wao ni Waislamu, dhidi ya Wakristu ambao ndiyo wengi nchini humo. "Ingawa wanajeshi wa Ufaransa na Umoja wa Afrika wameipa fursa nchi yetu kuwa na mwanzo mpya, maendelea yamekuwa ya taratibu sana na vikosi hivyo haviwezi kumudu mzigo huo pekee yao," walisema.

Walisema kuwasili kwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kutaondoa hisia za hofu na kuleta matumaini. taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, lakini moja ya maskini zaidi duniani, limeshuhudia kuongezeka kwa ghasia tangu kuondolewa madarakani kwa rais Francois Bozize kufuatia vita vilivyoongozwa na rais wa sasa Miche Djotodia, ambaye ndiye rais wa kwanza Muislamu kuiongoza Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ingawa rais Djotodia aliuvuja muungano wa Seleka, baadhi ya wanajeshi waliokuwa katika muungano huo walicharuka, na kusababisha miezi kadhaa ya mauaji, ubakaji na uchomaji moto majengo, na kusababisha wakristu kuunda makubdi ya kujilinda.

Baadhi ya ndugu za waathirika wa machafuko wakiwatizama wagonjwa wao katika kituo kilichowekwa na shirika la misaada la Madaktari wasio na mipaka MSF mjini Bangui.

Baadhi ya ndugu za waathirika wa machafuko wakiwatizama wagonjwa wao katika kituo kilichowekwa na shirika la misaada la Madaktari wasio na mipaka MSF mjini Bangui.

Nzapalainga na Layama walisema kuwa kuna kitisho cha kweli kuwa Waislamu watakumbana na ulipizaji kisasi mbaya, kufuatia vitendo vilivyokithiri vya ubakaji, uporaji na mauaji yanayofanywa na waasi wa zamani. "Tunahofu kuwa iwapo jamii ya kimataifa haitaitikia haraka, nchi yetu itatumbukia kizani," walisema na kuongeza kuwa watu milioni mbili -- au zaidi ya nusu ya raia wa nchi hiyo wanahitaji msaada wa dharura.

Wanajeshi wa Chad wauawa
Usiku wa kuamkia Alhamisi, wanajeshi sita wa kikosi cha Chad cha kulinda amani waliuawa katika makabiliano yaliyozuka katika mji wa Bangui. Msemaji wa jeshi la Chad Eloi Yao alisema wanajeshi hao waliuawa katika mazingira ya kutatanisha huku wengine 15 wakijeruhiwa.

Duru kutoka hosptali ya mji wa Bangui zilisema watu kadhaa wameuawa tangu siku ya Jumatano, huku afisa mmoja wa hosptiali hiyo akisema shirika la misaada la msalaba mwekundu limeleta miili kadhaa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afp
Mhariri: Bruce Amani

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com