Viongozi wa AU wakutana Misri | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 30.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Viongozi wa AU wakutana Misri

Mkutano wa kilele wa 11 wa Umoja wa kiafrika umefunguliwa mjini Sharm el Sheikh nchini Misri akishiriki pia rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ambae alichaguliwa tena hivi karibuni katika hali ya kutatanisha.

default

Rais wa Misri Hosni Mubarak, mwenyeji wa mkutano.

Mkutano huo ambao umehudhuriwa na viongozi wa nchi na serikali 53, umeanza leo asubuhi ukiwa umechelewa kidogo. Baada ya hotuba ya ufunguzi ya mwenyeji rais wa Misri Hosni Mubarak, mkutano huo umeendelea faraghani. Miongoni mwa maada zilizopangwa kuzungumziwa ni pamoja na usalama, maji na mabadiliko ya hali ya hewa. Mbali na maada hizo, swala la Zimbabwe linatarajiwa kuchukua nafasi kubwa kwenye mazungumzo hayo baada ya rais Mugabe kuendelea na uchaguzi licha ya mpinzani wake Morgan Tsvangirai kujitoa kufuatia mashambulizi dhidi ya wafuasi wake na ambayo kwa maoni ya nchi nyingi hususan za magharibi hayakuruhusu uchaguzi huo kuwa huru na wa haki, kukiwa na uwezekano wa kuiwekea vikwazo serikali ya rais Mugabe.

Rais Mugabe baada ya kuapishwa hapo jana, anashiriki katika mkutano huo wa Umoja wa Afrika. Yeye anashikilia msimamo wake na kwamba Umoja wa Afrika hauna haki ya kumuwekea vikwazo: ´´Umoja wa Afrika hauna haki ya kutulazimisha namna ya kutumia katiba yetu. Kwa muda wote tutakuwa tunaheshimu sheria zetu, ningependa watuachie amani. Kama ni vikwazo, waache waweke, tutapata namna ya kueshi´´.

Katika shughuli za maandalizi ya mkutano huo zilizoanza ijumaa siku ya duru ya pili ya uchaguzi nchini Zimbabwe, mawaziri wa mambo ya kigeni walishindwa kufikia mwafaka juu ya hatua ambayo inafaa ichukuliwe serikali ya rais Mugabe na kuliachia swala hilo viongozi wao kuamua.

Lakini wadadisi wa mambo ya kisiasa hawategemei sana kuwa viongozi wa kiafrika wanaweza wakamchukulia hatua kali rais Mugabe kwani baadhi ya serikali nazo pia zina matatizo kama hayo kama anavyosema Moeletsi Mbeki, naibu mkurugenzi wa taasisi ya uhusiano wa kimataifa nchini Afrika ya kusini :´´Serikali za kiafrika zinaona haya kuchukuwa hatua kwa sababu nyingi ya hizo zinafanya vitu vibaya. Kwa hiyo inakuwa vigumu kuikosoa serikali nyingine kwa mfano Mugabe kwani wakifanya hivyo, watakuwa wameweka hadharani makosa yao. Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa muda wa miaka minanne. Halikujitokeza wiki chache zilizopita bali lipo tangu mwaka 2000´´

Mbali na viongozi wanaopendekeza vikwazo, kuna wengine wanaopendekeza kuimarisha upatanishi kumsaidia rais wa Afrika ya kusini Thabo Mbeki ambae amekuwa akifanya kazi hiyo kwa niaba ya jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC. • Tarehe 30.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ETN3
 • Tarehe 30.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ETN3
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com