1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la mpito Sudan laongezewa muda kutekeleza demokrasia

Angela Mdungu
23 Aprili 2019

Viongozi wa nchi za kiafrika wamekubaliana kuuongezea muda uongozi wa Baraza la mpito la kijeshi la Sudan ili liweze kutekeleza marekebisho ya demokrasia

https://p.dw.com/p/3HIRB
Ägypten Kairo - Gipfeltreffen
Picha: Reuters/The Egyptian Presidency

Uamuzi huo unatoa nafasi ya kuongeza muda kutoka siku 15, ambazo Umoja wa nchi za kiafrika ulilipatia baraza hilo la mpito la Sudan kuunda serikali ya kiraia hadi baada ya miezi mitatu

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi ameitaka jumuia ya kimataifa kuiunga mkono Sudan wakati ikipitia mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa baada ya aliyekuwa Raisi wa nchi hiyo Omar al Bashir kuondolewa madarakani. Akifungua mkutano kuhusu Sudan mjin Cairo, Rais Al Sisi amesema jumuiya ya kimataifa haina budi kuweka mazingira ya amani wakati wa huu wa mabadiliko ya kidemokresia ambayo raia wa Sudan wameyataka.

Rais Al Sisi amesema Jumuiya ya kimataifa inalo pia jukumu muhimu la kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi unaoendelea Sudan  jambo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa kinyume na matarajio ya raia wa nchi hiyo. Baadhi ya marais wa nchi za kiafrika, wakiwemo wa Rais Idriss Deby wa Chad,  Paul Kagame wa Rwanda, Denis Sassou-Nguesso wa Congo,  Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika ya Kusini na Ismail Omar Guelleh wa Djibouti. Mkutano huo umehudhuriwa pia  na Mwenyekiti wa Umoja wa nchi za ki Afrika  Moussa Faki.

Rais Al sisi ameeleza sababu ya viongozi hao kufanya mazungumzo kuwa ni kuangalia hali inavyoendelea Sudan na namna ya kuunga mkono waia wa Sudan katika juhudi za kurejesha matumaini yao na kuwaandaa vema kwa ajili ya maisha yao ya baaday huku wakizingatia juhudi za baraza la mpito la kijeshi pamoja na pande zote za kisiasa katika kuleta mapatano na kutafuta namna ya kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia kwa njia ya amani.

Ägypten Präsident Abdel Fattah el-SisiAbdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah el SisiPicha: picture-alliance/AP Images/AP Photo/E. Vucci

Awali Baraza hilo lilisema linahitaji muda wa miaka miwili ili kusimamia kipindi cha mpito kabla ya kuunda serikali ya kiraia itakayoundwa na wanataaluma.

Libya nayo yajadiliwa 

Nao mkutano wa pili wa kuijadili Libya ambao unawakutanisha viongozi wa Rwanda, Afrika ya Kusini na Kongo mjini Cairo utaangazia zaidi kuzindua upya hali ya kisisa ya taifa hilo pamoja na kutokomeza ugaidi. Libya imekuwa katika machafuko tangu kuondolewa na kuuawa kwa Kanali Muamar Ghadafi mwaka 2011 huku juhudi za kimataifa za kuiunganisha tena nchi hiyo iliyogawanyika zikigonga mwamba.

Wakati huohuo, shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba waandamanaji kutoka eneo alikozaliwa aliyekuwa Rais wa Sudan Omar Al Bashir wameelekea mji mkuu Khartoum huku maandamano zaidi yakiendelea nchi nzima. Kwa mujibu wa wanaharakati huo ni mwendelezo wa juhudi za kushinikiza kuundwa kwa serikali ya kiraia.

Mwandishi: Angela Mdungu/DPAE/APE/AFPE

Mhariri: Sekione Kitojo