Viongozi wa Afrika wakamilisha mkutano wao | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Afrika wakamilisha mkutano wao

Changamoto ya mizozo bado inawakabili

Rais wa Malawi Bingu Wa Mutharika, mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika

Rais wa Malawi Bingu Wa Mutharika, mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika

Viongozi wa Afrika hii leo wamekamilisha mkutano wao mjini Addis Ababa nchini Ethiopia bila kuwepo na tofauti kubwa miongoni mwao na wakiwa na matumaini ya kuimarisha uchumi wa bara zima la Afrika. Hata hivyo Umoja wa Afrika bado unakabiliwa na msururu wa mizozo inayosubiri kupatiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na kujitenga kwa Sudan Kusini kutoka kwa utawala wa Khartoum.

Kamisha wa baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra amesema hii leo kwamba azimio lililoidhinishwa usiku wa kuamkia leo linaloongeza shinikizo dhidi ya kiongozi wa Madagascar, Andry Rajoelina, aliyenyakua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi na ambaye hakuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika huko mjini Addis Ababa Ethiopia. Viongozi wa Afrika wamewataka viongozi wanaohasimiana nchini Madagascar waheshimu makubaliano yaliyofikiwa kwa lengo la kuutanzua mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo.

Hali nchini Sudan ambako wasiwasi unazidi huku kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika mwaka ujao 2011 ikikaribia, ilikuwa miongoni mwa mada zilizopewa kipaumbele katika ajenda ya mkutano wa mjini Addis Ababa. Katika kura hiyo ya maoni inatarajiwa kwamba Sudan Kusini itapiga kura kutaka uhuru wake kutoka kwa serikali ya mjini Khartoum.

Kamisha wa baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra, amesema hali nchini Sudan imejadiliwa kwa kina kwenye kikao maalum kilichofanyika pembezoni mwa mkutano wa mjini Addis Ababa ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, rais wa Sudan Omar al Bashir na waziri mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi walishiriki. Marais wa Afrika Kusini, Algeria na Chad pia walikuwepo katika kikao hicho maalum. Bwana Lamamra amesema kikao hicho kilikuwa muhimu na kwamba wanajiandaa kuchukua hatua.

"Swala la Sudan limejadiliwa kwa kina. Tutazingatia hatua zote za kuchukuliwa kulingana na ugumu wa hali ilivyo na umuhimu wa kushirikiana pamoja bila ya kuzingatia matokeo ya kura ya maoni ya Januari 9 mwaka 2011. Amani haitahatarishwa; na maridhiano yaliyopatikana katika mkataba wa mwaka 2005 hayatapigwa teke na kuzusha mzozo na vita."

Abdoulaye Wade

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade amewatolea mwito viongozi wa Afrika kuungana pamoja katika vita dhidi ya kitengo cha kundi la al Qaeda kilichoko Afrika Kaskazini. Amesema nchi kama Senegal au Mali haziwezi kufanya kitu chochote dhidi ya al Qaeda na kuyataka mataifa ya magharibi yaingilie kati kusaidia kwa kuwa tatizo la al Qaeda ni la kimataifa.

Kuhusu uchumi, wataalam wamesema wanaona dalili za uchumi wa bara la Afrika ukianza kuimarika tena. Mkuu wa benki ya maendeleo ya Afrika, ADB, bwana Donald Kaberuka, raia wa Rwanda, anatarajia uchumi wa Afrika kukua kwa kati ya asilimia 4.5 na asilimia 5 mwaka huu. Amebashiri uchumi wa Afrika utakua kwa asilimia 6 mwaka ujao 2011. Hata hivyo kiongozi huyo ameonya kwamba matatizo ya kiuchumi barani Afrika hayajatatuliwa kikamilifu.

Mwandishi: Charo Josephat/ AFP

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed

 • Tarehe 02.02.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LprS
 • Tarehe 02.02.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LprS
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com