Viongozi wa Afrika kumuaga rasmi Mugabe mjini Harare | Matukio ya Afrika | DW | 14.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Viongozi wa Afrika kumuaga rasmi Mugabe mjini Harare

Viongozi mbalimbali wanakusanyika mjini Harare kumpa buriani rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

Viongozi mbalimbali wa Afrika wanatarajiwa kuhudhuria hafla rasmi ya kitaifa ya kumuaga rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe, katika uwanja wa kitaifa mjini Harare.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, na viongozi wengine walioko madarakani kwa sasa na wa zamani ni miongoni mwa wale wanaotarajiwa kuhudhuria hafla hiyo katika uwanja wa Rufaro.

Hata hivyo mazishi kamili ya Mugabe yatafanyika mwezi ujao baada ya kumalizika kwa ujenzi wa kaburi lake, katika eneo la makaburi ya mashujaa wa kitaifa. Hayo yamesemwa na familia yake .

Hapo kesho, mwili wa Mugabe utasafirishwa hadi kijijini kwao Zvimba, ili tambiko za kitamaduni zifanywe na pia mazishi ya ishara kabla ya mazishi kamili mwezi ujao.

Mugabe aliyefariki wiki iliyopita nchini Singapore akiwa na umri wa miaka 95, ameacha Zimbabwe ikiwa na hisia mseto kuhusu utawala wake wa miaka 37, uliohusishwa na mkono wa chuma pamoja na shida za kiuchumi

Aliaga dunia takriban miaka miwili kamili tangu jeshi kumlazimisha kujiuzulu mwaka 2017, kufuatia mzozo wa madaraka kuhusu kile kilichotizamwa kuwa njama ya kutaka mke wake Grace kumrithi madarakani.

Mfuasi wa rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwa amebeba kitambaa chenye mchoro wa Mugabe katika uwanja wa Rufaro anakoagwa Mugabe.

Mfuasi wa rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwa amebeba kitambaa chenye mchoro wa Mugabe katika uwanja wa Rufaro anakoagwa Mugabe.

Mwili wake ulirejeshwa nchini Zimbabwe kutoka Singapore siku ya Jumatano.

Zimbabwe imegawika na ingali inakumbwa na mfumko wa bei ya bidhaa, pamoja na uhaba wa chakula na mafuta kufuatia miongo mingi ya utata wa kiuchumi.

"Licha ya baadhi ya mashaka juu yake pamoja na yale yanayotajwa kuwa makosa au mapungufu yake.. msimamo wa serikali ni wazi. Ras wa zamani wa Zimbabwe obert Mugabe ni shujaa. " Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Zimbabwe Sibusiso Moy aliliambia shirika la habari la AFP.

Japo Mugabe alimaliza utawala wa Wazungu walio wachache, na kuwapa Waafrika ambao ni wengi nafasi ya kupata huduma za afya na elimu, aligeuka na kuanza kuendeleza hofu na ukandamizaji katika utawala wake.

Wazimbabwe wengi watamkumbuka Mugabe zaidi kwa usimamizi mbaya wa uchumi na utawala wa mkono wa chuma uliofuata matumaini ya awali ya kuwa mkombozi.

Mamilioni ya watu walikimbia Zimbabwe baad ya miongo kadhaa ya mfumko wa bei na operesheni za kikatili dhidi ya wakosoaji.

Vyanzo: AFPE, APE