1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUhispania

Vinícius Junior aishtumu La Liga kwa kutopambana na ubaguzi

22 Mei 2023

Vinicius Junior ameishtumu vikali Ligi Kuu ya Uhispania La Liga na kueleza kwamba, "ligi hiyo ni ya wabaguzi wa rangi" baada ya kutupiwa maneno ya kibaguzi na mashabiki wakati wa pambano dhidi ya Valencia.

https://p.dw.com/p/4Rg82
Fußball | Valencia CF v Real Madrid CF - LaLiga Santander
Picha: Jose Breton/NurPhoto/picture alliance

Kupitia mtandao wake wa Instagram, raia huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 22, ameandika, "Wakati fulani La Liga ilipambwa na akina Ronaldinho, Cristiano Ronaldo, Lionel Messi ila leo Ligi hii imejaa wabaguzi."

Rais wa Brazil Luiz Lula da Silva amelaani ubaguzi huo wa rangi, na amewaambia waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano wa kilele wa mataifa ya G7 mjini Hiroshima Japan kwamba, Vinicius Junior aliitwa "nyani."

Winga huyo amekuwa akilengwa mara kwa mara na matusi ya ubaguzi wa rangi miaka mitano tangu alipojiunga na miamba hao wa Uhispania, japo kumefanyika juhudi ndogo kukabiliana na hali hiyo.

Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelloti amesema,"Kilichotokea leo, kimetokea pia mara nyingi, lakini hakifai kuendelea tena. Hapana. Hii haikubaliki. Ligi Kuu ya Uhispania ina tatizo na wala sio Vinicius. Vinicius ni mhanga. Tatizo la ubaguzi wa rangi ni kubwa sana."

Mwezi uliopita, tume ya kupambana na ghasia ilipendekeza faini ya euro 4,000 na kupigwa marufuku kwa miezi 12 kwa shabiki ambaye alimuita Vinicius "nyani" katika mechi ya ligi dhidi ya Mallorca.