1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vilabu kujikatia tikiti ya fainali ya Champions League

4 Mei 2015

Ligi ya mabingwa barani Ulaya - Champions League inarejea viwanjani Jumanne na Jumatano katika michuano ya kukata na shoka ya kutafuta tikiti ya kucheza katika fainali ya Berlin, Ujerumani

https://p.dw.com/p/1FJz0
Kombo Robben Messi WM Halbfinale Vorschau
Picha: Odd Andersen/AFP/Getty Images

Real Madrid baada ya kupambana kuuvunja ukuta mgumu miongoni mwa timu za Ulaya katika robo fainali dhidi ya Atletico Madrid , kesho Jumanne inaingia tena uwanjani kuwania kuvunja ukuta mwingine mgumu zaidi wa Juventus Turin.

Mabingwa hao watetezi walitumia chini ya saa tatu kuuvunja upinzani wa Atletico Madrid, kwa ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa pili wa duru hiyo.

Hata hivyo Juventus ya Italia ni timu bora zaidi ya Atletico , na ina uwezo wa kusogea mbele na kushambulia iwapo nafasi inapatikana.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Karem Benzema hakusafiri na kikosi hicho kwenda Turin , wakati Gareth Bale yumo kikosini baada ya kurejea kundini baada ya matatizo ya paja.

Lakini shughuli iko upande wa Pep Guardiola na kikosi chake cha Bayern Munich , ambapo Pep anafika kwa mara ya kwanza Camp Nou akiwa upande wa benchi la upinzani, na timu yake Bayern Munich ikiwa na majeruhi lukuki.

Barcelona inaonekana kuimarika kila wakati na wachezaji wote wako fit kwa mchezo huo wa Jumatano. Mshambuliaji hatari wa Bayern Munich Robert Lewandowski hana hakika ya kucheza katika mchezo huo baada ya kuvunjika taya na pua katika mchezo dhidi ya Borussia Dortmund katikati ya wiki , na Pep Guardiola anawakosa wachezaji wake muhimu, kama David Alaba, Arjen Robben , Frank Ribery na Holger Badstuber.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae /
Mhariri: Daniel Gakuba