1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikundi vya kijamii vyatetea wakulima nchini Cameroon.

3 Desemba 2006

Makundi ya kijamii nchini cameroon yameeleza wasi wasi wao kuhusu athari za kufungua milango ya biashara zitakazowakumba wakulima wa Cameroon katika eneo la Afrika ya kati , kuhusu usalama wa chakula. Sekione Kitojo na taarifa kamili.

https://p.dw.com/p/CHm2

Makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi EPAS, baina ya umoja wa Ulaya na mataifa yanayoendelea yataruhusu mataifa hayo ya Ulaya kujaza bidhaa zao za kilimo katika soko la Cameroon , baadhi ya bidhaa hizo zikiwa zinatolewa ruzuku na serikali, amesema mtaalamu wa masuala ya fedha Celestin Nkou Nkou katika mji mkuu Yaounde.

Majadiliano hayo ya EPAS yalianza katika mataifa yanayounda sehemu ya jumuiya ya uchumi na fedha ya Afrika ya kati Septemba mwaka jana , mazungumzo ambayo yanalenga katika kufufua ushirikiano baina ya umoja wa Ulaya na mataifa ya Afrika , Caribbean, na pacific ACP, ushirika ulioanzishwa katika miaka ya 1970.

Inatarajiwa kuwa mataifa hayo ya ACP yatafungua masoko yao kikamilifu kwa bidhaa za kilimo za mataifa ya Ulaya chini ya makubaliano hayo yanayopitiwa upya, amesema Nkou Nkou.

Lakini anadokeza Joyce Mbowen wa chama cha wafanyakazi wa kilimo kuwa uhuru wa kuwa na chakula chetu wenyewe , ambao tayari umeingia katika msukosuko kutokana na uingizaji hivi karibuni kutoka Ulaya wa nyama ya kuku, viazi vikuu, mchele, sukari , unga na bidhaa nyingine za chakula kutoka mataifa mengine , unakandamiza dhamira hii.

Baada ya mapambano yaliyoanzishwa mwezi wa Juni kusitisha uingizaji wa nyama ya kuku kutoka Ulaya , makundi ya kijamii yametoa wito kwa bunge la Cameroon kujiunga na makundi hayo na kuwaunga mkono wakulima na kulinda uzalishaji wa chakula kutoka nchini humo.

Wakati mbunge Josephine Elingui anaamini kuwa suala hili ni muhimu sana, amesema pia kuwa halitashughulikiwa hadi mwezi March 2007 wakati wa kikao kingine cha bunge, wakati majadiliano mwezi uliopita yalituwama zaidi kwa ajili ya bajeti ya taifa.

Pamoja na hayo ameliambia shirika la habari la IPS kuwa wabunge wamependekeza kwa wizara ya kilimo na maendeleo vijijini , kutoa mikopo zaidi midogo midogo kwa wakulima , ili kufufua sekta ya uzalishaji wa kilimo kwa ufanisi zaidi.

Katika wakati huu wakulima nchini humo hawana uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha. Paul Nyobe, makamu rais wa chama kikuu cha wakulima , chenye makao yake makuu mjini Yaounde , amesema kuwa kilimo nchini Cameroon kinakabiliwa na matatizo ya kutokuwa na uongozi sahihi, na kushindwa kupata mikopo pamoja na mafunzo ya kiufundi.

Ili kupunguza pengo katika uzalishaji wake wa chakula mwaka huu Cameroon iliagiza kutoka nje tani 51,647 za samaki wabichi na tani 29,120 za kuku waliohifadhiwa kwa barafu kutoka mataifa ya Ulaya magharibi. Tani 48,790 za viazi vikuu kutoka Nigeria pamoja na maharage kutoka Senegal, kwa mujibu wa wizara ya biashara.

Takwimu zilizotolewa mwezi uliopita na wizara ya kilimo zinaonyesha kuwa nchi hiyo imekuwa ikiagiza tani 250,000 za mchele kila mwaka kutoka India, Pakistan na China na kiasi cha tani 190,000 za ngano katika muongo mmoja uliopita . hata hivyo kiasi kikubwa cha bidhaa hizo zinazoagizwa kutoka nje pamoja na bidhaa nyingine za kilimo kutoka nchini humo zinasafirishwa tena nje katika mataifa mengine ya eneo la karibu, wanasema maafisa.

Pierre Massock kutoka wizara ya kilimo ya Cameroon anasema kuwa mkakati wa serikali kwa ajili ya sekta ya vijijini iko katika msingi wa shughuli za maendeleo ya uzalishaji wa mboga mboga, mbegu bora na kuhimiza kuwa na hifadhi ya chakula katika eneo la kaskazini ya nchi hiyo. Ameongeza kuwa mkakati huu pia utasaidia katika kuanzisha upya mtandao imara wa kilimo na kuhimiza uzalishaji katika kilimo kupitia kilimo cha kisasa kinachotumia matrekta