1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Iraq vyapenyeza zaidi mji wa Mosul

4 Novemba 2016

Vikosi vya Iraq vimedhibiti tena wilaya sita,mashariki mwa mji wa Mosul nchini Iraq zilizokuwa chini ya himaya ya  kundi linalojiita dola la kiislamu IS ,siku moja baada ya kiongozi wa kundi hilo kuapa hawarudi nyuma.

https://p.dw.com/p/2SAzF
Irak Armee im Vormarsch auf Mossul
Picha: picture-alliance/dpa/A. Jalil

Kamanda wa  kitengo maalum cha kukabiliana na ugaidi anayeongoza mashambulizi hayo amesema vikosi vyake vimefanikiwa kuzingira eneo kubwa waliko wapiganaji  hao wa IS.Vikosi hivyo vya Iraq vimechukua udhibiti wa eneo la Malayeen, Samah, Khadra,Karkukli,Quds na Karama katika mashambulizi yaliyosababisha hasara kubwa  kwa wapiganaji wa IS.Vikosi hivyo kisha viweka Bendera ya Iraq katika majengo yaliyokuwa yakisimamiwa awali na wapiganaji hao.Sehemu iliyotekwa na vikosi vya serikali  ni kipande tu cha mji huo wa Mosul ambao umegawanywa maeneo ya makaazi  na viwanda.Mji huo ambao umekuwa chini ya usimamizi wa IS tangu mwaka 2014 una wakaazi millioni 2.

Bildergalerie ein Jahr Islamischer Staat in Mossul
Wakaazi wa Mosul katika soko maarufu lilo katikati mwa mji huoPicha: picture-alliance/epa/M. Al-Mosuli

Operesheni hiyo ya kuwatimua wapiganaji hao  kutoka mji wa Mosul ndio kubwa zaidi ya ardhini kuwahi kufanyika nchini Iraq tangu ile iliyoongozwa na Marekani mwaka 2003,na huenda ikaamua hatma ya wapiganaji hao wa IS ambao wamekaidi ulimwengu kwa kipindi cha miaka miwili. Shirika la Umoja wa mataifa  limesema wakati operesheni hiyo ikiendelea wapiganaji hao wameendelea kuwaua mamia ya watu ikiwa ni pamoja na wasiotaka kujiunga nao na wafanyikazi wa zamani 180 wa serikali ya Iraq.Kundi hilo pia limehusishwa na utekaji kwa mujibu wa Ravina Shamdasani  ambae ni msemaji wa ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu katika shirika hilo la Umoja wa mataifa "Tuna taarifa  kuwa wanamgambo  wa IS wanawazulia mateka  karibu akinamama 400 wa  Kikurdi,Yazidi  au  wale wa Kishia huko  Tal Afar. Tangu  Octoba  17 kundi hilo la IS  limeripotiwa kuwasajili kwa nguvu  watoto walio  umri wa miaka 9 au 10  kama wapiganaji katika mji wa Mosul."

Irak Regierungstruppen bei Mossul
Majeshi ya Iraq katika operesheni kusini mwa MosulPicha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Kufikia sasa maeneo yaliyotekwa na vikosi vya Iraq kutoka kwa IS hayana watu wengi  kama maeneo mengine,hasa ukanda wa magharibi wa mto Tigris ambao idadi kubwa ya watu wake ni Waisamu wa Kisunni na huenda pia wamekita mizizi  Wasunni wenye msimamo mkali .Vikosi vya Iraq na vile vya Marekani vinavyoendesha operesheni ya angani na ardhini vimesema vimefanikiwa kuindesha kwa haraka kuliko ilivyotazamiwa ,lakini vikashikilia bado operesheni hiyo imo katika hatua za kwanza.Shirika la Umoja wa mataifa limesema watu elfu 22 wametoroka makwao tangu kuanza kampeini hiyo ya kuukomboa mji wa Mosul,bila kuhesabu  maelfu ya wengine kutoka ijiji jirani vya na mji huo  waliolazimishwa kwenda Mosul na wapiganaji wa IS ili kuwatumia kama ngao.

 

Mwandishi:Jane Nyingi/RTRE/APE
Mhariri:Yusuf Saumu