1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya angani vya Ethiopia vyashambulia Mekele, Tigray

John Juma
26 Agosti 2022

Shambulizi la angani limetokea mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele, Ijumaa. Msemaji wa wapiganaji wa jimbo hilo na vyanzo kutoka mashirika ya kiutu wamesema hayo.

https://p.dw.com/p/4G61l
Tigray-Krise in Äthiopien
Picha: UGC/AP/picture alliance

Msemaji wa wapiganaji wa jimbo hilo pamoja na vyanzo kutoka mashirika ya kiutu wamesema hayo mnamo wakati serikali ikiapa kuchukua hatua dhidi ya kambi au maeneo ya kijeshi ya wapiganaji hao wa jimbo hilo linalokumbwa na machafuko. Serikali imekanusha madai kwamba imeshambulia maeneo ya raia bali wanalenga vituo vya kijeshi jimboni Tigray.

Hayo yamejiri mnamo wakati serikali ikiapa kuchukua hatua dhidi ya kambi au maeneo ya kijeshi ya wapiganaji wa jimbo hilo linalokumbwa na machafuko. 

Guterres azitaka Ethiopia na Tigray kusitisha mapigano mapya

Ripoti za shambulizi la angali zimejiri siku chache tu baada ya kuzuka kwa mapigano ya ardhini kati ya vikosi vya serikali ya shirikisho la Ethiopia na waasi, miezi mitano tu tangu mapigano hayo kutulia. Mapigano hayo ya sasa yameuvunja mkataba uliokuwepo wa kusitisha vita pamoja na matumaini ya mazungumzo ya amani.

Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF, kimesema eneo la makaazi ya watu pamoja na shule ya chekechea, yalilengwa kwenye shambulizi la kwanza la angani dhidi ya jimbo hilo ambalo limekuwa likishikiliwa na waasi kwa miezi mingi.

Wapiganaji wa TPLF washangilia walipoukomboa tena mji mkuu wa Tigray Mekele mikononi mwa jeshi la Ethiopia Juni 2021.
Wapiganaji wa TPLF washangilia walipoukomboa tena mji mkuu wa Tigray Mekele mikononi mwa jeshi la Ethiopia Juni 2021.Picha: Million Haile Selassie/DW

Msemaji wa TPLF Kindeya Gebrehiwot ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya ujumbe kwamba "raia wameuawa, wengine wamejeruhiwa na kwamba operesheni ya uokozi inaendelea.

Duru kutoka mashirika mawili ya kiutu zimelieleza shirika hilo la habari kwamba, walikuwa wameambiwa kuhusu shambulizi la angani mjini Mekele, lakini hakukuwa na maelezo zaidi kuhusu maeneo haswa yaliyoshambuliwa na kwamba taarifa kuhusu idadi ya watu waliouawa haikuwa imepatikana mara moja.

Ethiopia yailaumu TPLF kwa kutoshirikiana kutafuta amani

Muda mfupi tu baada ya ripoti za shambulizi hilo kutokea, serikali ilitangaza kwamba "itachukua hatua dhidi ya TPLF. Aidha iliwatahadharisha raia kujiepusha na maeneo ambayo jeshi linalenga katika jimbo hilo la kaskazini.

Kupitia tarifa, idara ya mawasiliano ya jeshi la shirikisho imesema "wakati utayari wa serikali ya shirikisho kuzungumza bila masharti ukihifadhiwa, itachukua hatua inayolenga vikosi vya jeshi".

Imesema inalenga tu vituo au maeneo ya kijeshi katika jimbo hilo la Tigray, hivyo kukanusha madai ya waasi kwamba shambulizi la angani limelenga maeneo ya raia katika mji mkuu wa jimbo hilo Mekele.

Baadhi ya makaburi ya pamoja ya watu waliouawa kufuatia machafuko majimbo ya Tigray na Afar. Kulingana na ripoti za idara ya afya eneo hilo, raia 58 walizikwa kwenye makaburi hayo.
Baadhi ya makaburi ya pamoja ya watu waliouawa kufuatia machafuko majimbo ya Tigray na Afar. Kulingana na ripoti za idara ya afya eneo hilo, raia 58 walizikwa kwenye makaburi hayo.Picha: Mariel Müller/John Irungu/DW

Taarifa ya serikali imeongeza kuwa chama cha TPLF kimeanza kutupa mifuko bandia ya maiti katika maeneo ya raia ili wadai kuwa vikosi vya serikali vimeshambulia raia.

Waasi wa Ethiopia wanasema serikali haiwezi 'kuaminiwa'

Mnamo mwezi Machi makubaliano ya kusitisha vita yalituliza mapigano yaliyosababisha umwagaji damu na kuruhusu misafara ya magari ya misaada kuanza tena kupeleka misaada Tigray. Umoja wa Mataifa umesema mamilioni ya wakaazi wa jimbo hilo wanakabiliwa na njaa kali huku kukiwa pia na upungufu mkubwa wa mafuta na dawa.

Mnamo Jumatano wiki hii, pande hizo mbili kwenye mgogoro huo, zilitangaza kuanza tena kwa mapambano, huku kila upande ukiutuhumu mwingine kwa kuanziasha mashambulizi katika mpaka wa kusini mwa jimbo hilo.

Maelezo kamili hayajabainika, lakini inaonekana mapigano hayo hayajaenea hadi nje ya eneo la mpaka kati ya Tigray na Amhara na Afar.

Kurejea tena kwa mapigano kumeitia wasiwasi jamii ya kimataifa ambayo imekuwa ikifanya juhudi kutaka pande hizo mbili kuafikiana kwa njia ya amani kuumaliza mzozo huo ambao umedumu kwa miezi 21, katika taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Watu milioni 20 nchini Ethiopia wanakabiliwa na baa la njaa

Waziri Mkuu Abiy Ahmed katika Makao Makuu ya Vikosi vya Ulinzi mjini Addis Ababa Ethiopia. (Picha ya maktaba 09.01.2022)
Waziri Mkuu Abiy Ahmed katika Makao Makuu ya Vikosi vya Ulinzi mjini Addis Ababa Ethiopia. (Picha ya maktaba 09.01.2022)Picha: Seyoum Getu/DW

Tangu mwisho wa mwezi Juni, serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed pamoja na wakuu wa Tigray wamekariri utayari wao kushiriki mazungumzo ya amani, lakini wamekuwa wakitofautiana kuhusu masharti ya mazungumzo hayo.

Aidha katika wiki za hivi karibuni, pande hizo zimeshutumiana kwa kujiandaa kurudi kwenye mapambano.

Mnamo Novemba 2020, Abiy Ahmed alituma vikosi vyake, kuondoa madarakani chama cha TPLF akikituhumu chama hicho kinachotawala jimbo hilo kwa kupanga mashambulizi dhidi ya vituo vya jeshi la serikali ya shirikisho.

Kilichofuata ni miezi ya uhasama kati ya Addis Ababa na chama cha TPLF ambacho kilitawala siasa za Ethiopia kwa miongo mitatu hadi pale Abiy alipochukua madaraka mwaka 2018.

(AFPE, RTRE)