Vikosi vya Afrika vinatosha kulinda amani Dafur. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 13.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Vikosi vya Afrika vinatosha kulinda amani Dafur.

Mataifa ya Afrika yameahidi kutowa vikosi vya kutosha kulinda amani huko Dafur kwa hiyo hakuna haja ya kuwahusisha wanajeshi wa kulinda amani wa kutoka nje ya bara hilo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Alpha Oumar Konare.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Alpha Oumar Konare.

Hayo yametamkwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika AU Alpha Oumar Konare hapo jana kauli ambayo yumkini ikazusha utata mpya kufuatia kuidhinishwa hivi karibuni na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kikosi mchanganyiko cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kulinda amani huko Dafur nchini Sudan.

Alpha Oumar Konare amesema baada ya kukutana na Rais Omar al Bashir wa Sudan mjini Khartoum kwamba baada ya kupokea ahadi kutoka nchi za Afrika hawana haja ya kuchukuwa vikosi visivyo vya Afrika.

Konare ameongeza kusema kwamba wana vikosi vya kutosha vya Afrika kwa ajili ya kuwekwa Dafur kulinda amani kwenye jimbo hilo la magharibi mwa Sudan lenye vurugu.

Kuna wanajeshi wapatao 7,000 kutoka nchi 26 za Afrika ambao hivi sasa wanashiriki kwenye kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika huko Dafur ambacho kimewekwa hapo mwezi wa Augusti mwaka 2004.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Julai 31 lilidhinisha upelekaji wa kikosi mchanganyiko cha wanajeshi na polisi 26,000 wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kulinda amani huko Dafur ambako zaidi ya watu 200,000 wameuwawa na wengine zaidi ya milioni mbili kupotezewa makaazi kutokana na mzozo wa miaka minne.

Konare amesema kwamba vikosi kutoka nje ya Afrika vitakuwa tu vinahitajika iwapo nchi za Kiafrika zitashindwa kutimiza ahadi zao za kutowa wanajeshi.

Ameongeza kusema kwamba hivi sasa zinahitajika fedha za kutosha kugharamia uwekaji wa kikosi hicho cha Afrika na kwamba anaamini mpira sasa uko katika Uwanja wa Umoja wa Mataifa ambao umaeahidi kugharamia operesheni hiyo.

Tangazo hilo la Konare linakwenda kinyume na taarifa iliotolewa hapo Jumanne na mjumbe wa Marekani kwa Sudan Andrew Natsios kwamba serikali ya Sudan itabidi kukubali vikosi visivyo vya Kiafrika katika kuimarisha kikosi cha kulinda amani huko Dafur kwa sababu bara la Afrika halina wanajeshi wa kutosha waliopatiwa mafunzo kuunda kikamilifu kikosi hicho cha kulinda amani.

Muundo wa kikosi cha kulinda amani ilikuwa ni sababu kuu ya kuchelewa kutolewa idhini ya Umoja wa Mataifa kutuma vikosi huko Dafur licha ya kuongezeka kwa shinikizo dhidi ya serikali ya Sudan kukubali kikosi hicho cha kimataifa.

Mkuu huyo wa Umoja wa Afrika pia ametangaza kwamba mkutano wa kimataifa juu ya suala la Dafur utafanyika mjini New York Marekani hapo mwezi wa Septemba na utadhaminiwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Rais Bashir wa Sudan ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipiga dhima yoyote ile muhimu ya Umoja wa Mataifa huko Dafur kwa hoja kwamba itakiuka haki yake ya kujitawala na kwamba inaweza kuifanya hali hiyo kuzidi kuwa mbaya ameunga mkono kauli hiyo ya Konare.

Bashir amesema baada ya mkutano wake wa Jumapili na Konare ambaye ameondoka Khartoum mara tu baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo kwamba wanaunga mkomo kikosi cha Umoja wa Afrika ambacho kinaimarisha juhudi za serikali ya Sudan za kuhakikisha kunakuwepo usalama,amani na utulivu katika jimbo la Dafur.

Katika mazungumzo yaliofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia yaliyowakutanisha wawakilishi wa Umoja wa Afrika,Umoja wa Waarabu,wanachama wa kudumu watano wa Baraza la Usalama, Misri,Umoja wa Ulaya halikadhalika maafisa waandamizi kutoka Congo na Gabon maendeleo makubwa yamefikiwa katika kupanga hatua za kusonga mbele kutokomeza umwagaji damu huko Dafur hususan kwa kupitia makubaliano juu ya uwekaji wa kikosi mchanganyiko cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwenye jimbo hilo.

 • Tarehe 13.08.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB20
 • Tarehe 13.08.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB20

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com