1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vigogo wapata vipigo Europa League

Admin.WagnerD15 Februari 2013

Awamu ya 32 ya Ligi ya Ulaya, Europa League ilitimua vumbi jana (14.2.2013) ambapo timu nne za Ujerumani Bayer Leverkusen, VfB Stuttgart, Hanovver 96 na Borussia Moenchengladbach zote zilishuka dimbani.

https://p.dw.com/p/17ee7
Picha: Reuters

Mambo hayakuwa mazuri kwa Bayer Leverkusen iliyokutana uso kwa uso na kikosi cha Benefica kutoka Ureno. Leverkusen ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa bao 1-0. Nayo Hannover 96 ilishindwa kufua dafu mbele ya Anzhi Makhachkala ya Urusi pale ilipolazimishwa kipigo cha bao 3-1.

Mambo hayakuwa mabaya kiasi kwa Borussia Moenchengladbach na VfB Stuttgart ambazo zote zilipata sare katika mechi za jana. Moenchengladbach iliyoumana na Lazio ya Italia ilitoka sare ya bao 3-3 wakati Stuttgart nayo iliangukia mkondo huohuo kwa matokeo ya bao 1-1 dhidi ya Genk ya Ubeligiji.

Christian Gentner wa VfB Stuttgart (watatu kulia) akifurahia ushindi dhidi ya KRC Genk
Christian Gentner wa VfB Stuttgart (katikati) akipachika bao dhidi ya KRC GenkPicha: Reuters

Matokeo ya juu kabisa kwenye mechi za usiku wa jana za awamu ya 32 ya Ligi ya Ulaya ni yale kati ya Borussia Moenchengladbach na Lazio, mchezo ambao pia zilipatikana penati tatu za nguvu.

Kati ya hizo penati ya kwanza na ya tatu ndizo zilizoingia wavuni Martin Stranzl wa Moenchengladbach ya Ujerumani alipiga mbili lakini akapata ya kwanza na kupoteza ya pili. Penati nyingine ilichezwa na Thobern Marx wa Lazio ya Italia ambayo bila shaka ilijaa wavuni.

Chelsea yapata pumziko la moyo

Michezo mingine iliyovuta hisia za mashabiki wa kandanda ni ile iliyoshirikisha vilabu vya Uingereza ambapo Tottenham Hotspur ilipambana na Lyon ya Ufaransa na matokeo kuwa ni bao 2-1. Mabingwa watetezi wa taji la Champions League, Chelsea walipata matumaini baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sparta Prague ya Jamhuri ya Czech.

Newcastle United ilicheza na FC Metalist Kharkiv ya Ukraine na kutoka sare ya 0-0. Nayo Liverpool ambao ni mabingwa mara tano wa mashindano haya ilipoteza mchezo wake na Zenit St. Petersburg ya Urusi kwa kufungwa mabao 2-0.

Usiku wa jana ulikuwa mzuri kwa Inter Milan ya Italia baada ya kuifunga bao 2-0 CFR Cluj ya Romania huku wenzao Napoli wakidoda kwa kufungwa magoli 3-0 na Viktoria Plzen Jamhuri ya Czech. Kwa upande wa Uhispania, Atletico Madrid ilisalimu amri kwa Rubin Kazan ya Urusi kwa kupachikwa mabao 2-0.

Wachezaji wa VfB Stuttgart wakifurahia ushindi dhdi ya KRC Genk
Wachezaji wa VfB Stuttgart wakifurahia ushindi dhdi ya KRC GenkPicha: Reuters

Kinachosubiriwa sasa ni awamu ya marudioano ambayo itatimua vumbi Alhamisi tarehe 21 Februari. Stuttgart itakutana na Genk ya Ubeligiji, Hannover 96 itakwaana tena na Anzhi Makhachkala, huku Bayer Leverkusen watapimana nguvu na Benfica ya Ubeligiji na kama kawaida Borussia Moenchengladbach itapambana na Lazio. Timu zote zilizochuana katika awamu hii ya 32 zitakutana tena siku hiyo.

Mwandishi: Stumai George/Ape/ Reuters

Mhariri: Josephat Charo