Vigogo wang′oke madarakani Bavaria | Magazetini | DW | 02.10.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Vigogo wang'oke madarakani Bavaria

Mashindano ya kuania madaraka katika chama cha CSU

Horst Seehofer anamezea mate vyeo vyote viwili chamani

Horst Seehofer anamezea mate vyeo vyote viwili chamaniHeka heka ndani ya chama cha Christian Social Union Union-CSU ndizo zilizomulikwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Mada nyenginezo ni pamoja na mswaada wa sheria uliopendekezwa na waziri wa sheriaq Brigitte Zypries kuhusu shughuli za usafiri.Mswaada huo wa sheria unalilazimisha shirika la usafiri liwalipe fidia watu kama treni zitakawia kufika kwa zaidi ya saa moja.


Tuanzie Munich lakini ambako gazeti la PASSAUER NEUE PRESSE linaanadika:Ni njambo la kustaajabisha kuona jinsi wanasiasa waliobobea wanavyokwepa kubeba dhamana ya madhambi yao.Katika wakati ambapo Erwin Huber kakubali shingo upande kufunga virago,mwenzake Günther Beckstein amejipurukusha kwa wakati wote hadi marafiki zake wenye ushawishi mkubwa walipomtanabahisha kwamba hata yeye enzi zake kama waziri mkuu zimekwisha.Ukweli huo unatia uchungu lakini hauepukiki.Kilichosalia sasa ni kutaraji tuu kwamba baada ya dhiki faraja.Wakubwa wakubwa ndani ya chama cha CSU wanashikilia pafikiwe makubaliano ya haraka ili Horst Seehofer akalie viti vyote viwili vya enzi ili kubainisha upepo unavuma upande gani.Lakini vuta nikuvute ndani ya kundi la chama cha CSu bungeni,lililoshindwa si kukubaliana kama Seehofer avikwe vilemba vyote viwili na wala kumteuwa mgombea mwengine,inaonyesha kukorofisha kila kitu.Kwa namna hiyo CSU wanajipotezea nafasi ya kuwavutia upya wapiga kura ambao wamechoshwa na vuta nikuvute isiyokwisha chamani."Gazeti la WESER-KURIER linawaambia wasomaji wake..."Karibuni katika msitu wa Bayrisch-Kongo.Vichwa vinafyekwa kufumba na kufumbua,na wanaopewa nafasi ya kutwaa madaraka wananoa visu zaidi.Yadhihirika kana kwamba suala la "nani katokea wapi" ndilo linalotangulizwa mbele.Watu wanaotokea sehemu ya Franken hawana nafasi nzuri ya kutwaa madaraka,wakilinganishwa na "wabavaria ya kale" au wa-Schwaben wanaoangaliwa kua ni wavumilivu.Ndo kusema wanatafakari chanzo cha matokeo mabaya ya uchaguzi"? Au huo ndio muongozo wa jinsi ya kuendelea kutawala? Hasha.Wana-CSU wanazozana wenyewe kwa wenyewe badala ya kujiuliza kwanini wapiga kura wamewapa kisogo?"


Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linaandika:


" Tsunami iliyofuatia zilzala iliyokitikisa chama cha CSU tangu ijumaapili iliyopita,imemng'owa pia Günther Beckstein madarakani.Hayo kwa kweli ndio matokeo ya maana baada ya pigo la uchaguzi.Kutokana na hali namna ilivyo ndani ya chama cha CSU hivi sasa,lingekua jambo la maana kama wadhifa wa kiongozi wa chama na ule wa waziri mkuu angekabidhiwa mtu mmoja tuu.Lakini Seehofer ana maadui wengi sawa na alivyokua na marafiki wengi chamani.Zaidi ya hayo kuna walakini nyengine pia:Nani atachjukua nafasi ya Seehofer mjini Berlin ili kutetea masilahi ya chama cha CSU katika daraja ya shirikisho?


Naam ,mada ya pili magazetini inahusiana na kuchelewa chelewa sana treni humu nchini.Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:


Kuanzia mwezi May mwakani watu wote wanaosafiri kwa treni watakua na haki kubwa zaidi-anasema waziri wa sheria Brigitte ZYPRIES.Treni ikikawia kuja kwa saa moja,abiria watabidi warejeshewe robo ya bei ya cheti cha usafiri,ikikawia kwa saa mbili watarejeshewa nusu ya bei hiyo.Ni jambo zuri hilo.Lakini bora tuseme tusibiri tuone hali itakuaje hasa.Kwasababu hata zamani shirika la usafiri wa reli liliwahi kuahidi kuwalipa fidia abiria wake.Lakini ahadi hizo zilisalia maneno matupu.Matumaini safari hii yanawekewa idara kuu ya safari za reli na kituo maalum cha kupokea malalamiko ya abiria kitakachoanzishwa na shirika la usafiri wa reli Deutsche Bahn .Taasisi hizo ndizo zitakazohakikisha,ahadi hizi mpya hazisalii karatasini.

 • Tarehe 02.10.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FStU
 • Tarehe 02.10.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FStU